NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe.Jamal Kassim Ali amesema kuwa,moja ya mkakati mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ni kuhakikisha kuwa, inatumia fursa zinazoizunguka nchi ili kukuza uchumi na kuwezesha wananchi kuwa na ustawi na uchumi bora.
Mheshimiwa Jamal ameyasema hayo leo Januari 10, 2022 wakati akiangazia kuhusu mikakati iliyopo katika kuhakikisha kila mwananchi anashiriki au kushirikishwa katika utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar.
Ni kupitia mjadala wa Kitaifa ulioandaliwa na Watch Tanzania kwa udhamini wa Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) ambao umeangazia mada inayohusu Dhana ya Mapinduzi ya Zanzibar na Falsafa ya Uchumi wa Buluu kupitia mtandao wa Zoom leo.
"Nchi inaelekea kusherehekea miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo yaliwafanya Wazanzibari wote kupata uhuru wao ikiwemo kisiasa na kijamii, lakini tukiwa tunaelekea kusherehekea miaka 58, tuna kazi kubwa kama Serikali na nchi na wananchi wote kufanya kuhakikisha tunafanya mapinduzi makubwa kiuchumi.
"Na moja ya mkakati mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Nane ni kuona namna gani tunatumia fursa tulizopewa na Mwenyenzi Mungu ya kuwa nchi yenye visiwa na bahari, yaani dhana nzima ya Uchumi wa Buluu ni namna gani tunazitumia fursa zake kukuza uchumi wetu na kuwawezesha wananchi kuwa na ustawi na maisha bora,"amesema Mheshimiwa Waziri Jamal.
Amesema kuwa, sekta hizo zinahusisha,uvuvi, huduma za kitalii ambazo zinaambatana na bahari, usafirishaji pamoja na mafuta na gesi ambayo yanapatikana ndani ya bahari.
Amesema kuwa, kitakwimu eneo ambalo lina mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar ni kupitia Uchumi wa Buluu.
Waziri amesema kuwa,Sekta ya Uvuvi kwa kipindi cha miaka mitatu imeweza kuchangia pato la nchi kwa asilimia 5 kuanzia 2018 hadi 2020.
Kwa upande wa Sekta ya Utalii, Mheshimiwa Jamal amesema kuwa, ilikuwa ikichangia kwa wastani asilimia 25 hadi 27 ya pato la nchi.
"Kwa hiyo ukiangalia ni nini mchango wake kwa uchumi na pato la nchi, utaona ni kwa namna gani hii Sekta ya Uchumi wa Buluu ilivyo na mchango mkubwa kwa nchi. Hata kwa upande wa ukuaji, Sekta ya Utalii inakuwa kwa kasi sana, hata kabla ya janga la UVIKO-19 kuja, sekta hii ilikuwa inakuwa kwa silimia 17,"amesema.
Amesema,Serikali ya Awamu ya Nane katika kuhakikisha fursa zilizopo zinakuwa na mafanikio zaidi walikuja na mkakati wa kuhakikisha wanaziainisha kwa kuwashirikisha wananchi na Sekta Binafsi ili waweze kufikia malengo haraka.