NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Alhaj Othman Masoud Othman, amesema ni muhimu kwa waumini wa dini ya kiislamu nchini kuwa na mipango madhubuti katika kutimiza wajibu wa uisalamu na kutekeleza ibada ya dini yao.
Alhaj Othman ameyasema hayo leo Januari 14,2022 alipowasalimia waislamu baada ya ibada ya Sala ya Ijumaa iliyoambatana na ufunguzi wa Masjid 'Aisha Bint Mohammed Ismail' huko Mwera Mkwajuni wilaya ya Magharib ‘A’ Unguja.
Amesema kwamba, ni lazima waislamu wazifanye nyumba za ibada kuwa ni taasisi muhimu za mashaurinano na mafumzo kwa vizazi na jamii kwa ujumla kwa kuweka mipango na utaratibu bora kupitia njia ya misikiti kwa nia ya kuendeleza ibada ya uislamu na jamii kwa jumla.
Aidha, ametaka waislamu kuendeleza uislamu wao kwa kuwa na utamaduni wa kutoa na kuchangia mali walizoruzukiwa kama njia sahihi ya uendelezaji wa dini yao, na kwamba kufanya hivyo ndio yanayojenga usialam na jamii kubaki na mshakamano na kuendeleza sifa bora ya dini hiyo.
Mapema, Katibu wa msikiti huo katika sala ya Ijumaa Sheikh Iddi Hussein Iddi, amekumbusha umuhimu wa waislam kuendeleza nyumba za ibada kama ilivyoelekezwa na Mola Muumba yakiwamo masuala ya utaoaji wa mafunzo na kufanya mashauri mbali mbali yanayohusu jamii.
Naye Mkurugenzi wa shirika la 'Al-nour charateble Organization for the Needy', Sherikh Nadir Makhfoudh, amesema kwamba shirika lake litaendelea kusaidia juhudi mbalimbali za waumini na wananchi kwa jumla katika kukuza na kuendeleza uislamu nchini kwa ujenzi wa misikiti, taasisi za mafunzo, kusaidia mayatima pamoja na jamii kwa jumla.