Benki Kuu ya Tanzania yawashirikisha Wanahabari njia bora za kuibua fursa za kiuchumi Nyanda za Juu Kusini

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa rai kwa waandishi wa habari kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini kuwa mstari wa mbele kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo hazijatumika ipasavyo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili ziweze kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Miongoni mwa mikoa katika nyanda hizo ni pamoja na Mkoa wa Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Njombe na Iringa ambayo imtejwa kuwa na fursa mbalimbali za kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Dkt. Bernard Kibesse katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Meneja Uchumi Tawi la Benki Kuu Mbeya, Dkt. Nicholaus Kessy.

Ni wakati akifungua semina ya Benki Kuu kwa waandishi wa habari za biashara, uchumi na fedha iliyoanza leo Februari 14, 2022 hadi Februari 18, 2022 katika Ukumbi wa Benki Kuu Tawi la Mbeya.

"Mikoa hiyo ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo hazijatumika ipasavyo ili kuchangia zaidi katika uchumi wa nchi yetu. Fursa hizo ni pamoja na ardhi nzuri ifaayo kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, hali ya hewa nzuri, pamoja na vivutio vingi vya utalii. 

"Waandishi wa habari pamoja na vyombo vyenu mna nafasi ya kuziibua fursa hizo kwa kuzitangaza ili kuwavuta wawekezaji na watalii kufika katika mikoa hii na kuchangia maendeleo ya nchi yetu. 

"Kwa mfano, Nyanda za Juu Kusini zina vivutio vingi vya utalii kama Mbuga za Taifa za Kitulo, Ruaha na Katavi, ambazo hazipati wageni wengi wa ndani na nje ya nchi pengine kwa sababu hazitangazwi sana,"amesema Dkt.Kibesse. 
Meneja Uchumi Tawi la Benki Kuu Mbeya, Dkt. Nicholaus Kessy kwa niaba ya Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Dkt. Bernard Kibesse akifungua semina ya waandishi wa habari waandamizi (hawapo pichani) wa vyombo vya habari nchini inayofanyika kwenye tawi la BoT mkoani Mbeya kulia ni Dorcas Mtenga Mwandishi mwandamizi wa Channel Ten na mwenyekiti wa semina hiyo kushoto ni Kaimu Meneja wa Uhusiano na Itifaki (BoT) Bi. Vick Msina.

Amefafanua kuwa, waandishi wa habari wakidahamiria kubadilisha hali hiyo wanaweza na kuifanya kanda hiyo iwe maarufu kama ilivyo Kanda ya Kaskazini kwa masuala ya utalii.

Dkt.Kibesse amesema kuwa,hivi karibuni limeibuka zao la parachichi, ambalo linahitajika sana siyo hapa nchini tu, bali pia nje ya nchi. 

"Pamoja na zao hilo, hali ya hewa katika Nyanda za Juu Kusini inaruhusu kilimo cha mbogamboga na matunda kwa soko la ndani na la nje. Kwa sasa, nyanda hii imejaliwa kuwa na uwanja wa ndege mkubwa ambao unaweza kutumika kwa ajili ya kusafirishia mazao hayo kwenda nje ya mikoa hii na hivyo kuwaongezea wananchi kipato. 

"Natoa wito kwa waandishi wa habari kutumia taaluma yenu kuhimiza wananchi kujishughulisha na kilimo cha mazao hayo na mengine kwa wingi ili kunufaika na fursa za masoko zilizopo. Kwa kufanya hivyo mtakuwa mnachangia kuongeza uzalishaji hapa nchini, kuwafanya wananchi wajiongezee kipato kutoka na mauzo ya mazao hayo na kuliwezesha taifa kupata fedha za kigeni kwa mazao yatakayokuwa yanauzwa nje ya nchi,"amefafanua Dkt.Kibesse. 
Wakati huo huo, Dkt. Kibesse amesema kuwa, Benki Kuu inapenda semina kama hizo zitumike kama fursa ya kuibua habari za kiuchumi zilizopo katika maeneo yenu. "Wananchi wanaposoma, kusikia au kuona shughuli za kiuchumi katika maeneo yao, wanahamasika kujiongeza kwa kufanya shughuli kama hizo au za aina hiyo kwa maendeleo yao na taifa letu.

"Pamoja na masuala ya shughuli za kiuchumi katika kanda hii, tunaamini kwamba elimu mtakayoipata kutoka kwa wawezeshaji wetu itawapa uelewa na uwezo mkubwa zaidi wa kuandika habari na makala mbalimbali kuhusu Benki Kuu ya Tanzania na masuala ya uchumi kwa ujumla. Mchango wenu unahitajika sana katika jitihada za Benki Kuu kuisadia Serikali yetu kufikia uchumi wa viwanda. Andika habari, makala na fanya mahojiano ambayo yatachangia kuelimisha umma juu ya haki zao za msingi na wajibu wao katika maendeleo ya taifa lao. 

"Ninapenda kuwahakikishia kwamba Benki Kuu itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kuhakikisha taarifa muhimu zinazotakiwa ziwafikie wananchi kutoka kwetu zinawafikia. Ofisi yetu ya Uhusiano wa Umma na Itifaki iko wazi wakati wote kuwahudumia, hivyo shirikiana nasi kwa maslahi mapana ya nchi yetu,"amefafanua Dkt.Kibesse.

Pia amesema kuwa, Benki Kuu ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na vyombo vya habari katika maendeleo ya taifa. 

"Aidha, tunazipongeza vyombo vya habari ambavyo, pamoja na mambo pengine, vina vipindi na makala maalum za habari za biashara, uchumi na fedha. Katika dunia ya sasa, maendeleo ya uchumi ndio kichocheo cha maendeleo katika nyanja zingine zote. Hivyo, kwa kutenga muda, vipindi, na nafasi kwa ajili ya habari za uchumi, biashara na fedha, vyombo vya habari vinachangia kuibua na kuuhabarisha umma fursa mbalimbali ambazo zikitumiwa zinachangia ukuaji wa uchumi.

"Tunafuatilia kwa makini habari na makala zinazohusu masuala ya uchumi na fedha zinazotolewa katika magazeti, redio, televisheni, na mitandao ya kijamii, , zikiwemo zinazohusu viwango vya ubadilishanaji wa fedha, biashara katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, minada ya dhamana za serikali na nyingine nyingi zinazohusu sekta ya fedha na uchumi, 

"Aidha, tunatambua na kuthamini sana mchango mkubwa unaofanywa na magazeti kutenga kurasa maalum za habari za fedha na uchumi, zikiwemo taarifa mbalimbali zinazotolewa na Benki Kuu, na pia vituo vya televisheni na redio mbalimbali kwa kuwa na vipindi maalum vya habari za uchumi, fedha na biashara.

"Kwa kiwango kikubwa Benki Kuu ya Tanzania inaridhika na jinsi vyombo vya habari vinavyotoa habari zinazohusu sekta ya fedha na uchumi.Hata hivyo, Benki Kuu inatambua kuwa vyombo vya habari na umma wa Kitanzania una hamu kubwa ya kuyajua mambo mbalimbali yanayohusu sera ya fedha na majukumu mbalimbali yanayonazoandaliwa na kutekelezwa na Benki Kuu ya Tanzania,"amefafanua Dkt.Kibesse.
Amesema kuwa, katika kujaribu kukabiliana na kiu hiyo kwa Watanzania na Wanahabari, tayari Benki Kuu ina kipindi maalum kila wiki cha ‘Ijue Benki Kuu ya Tanzania’ kinachorushwa na televisheni ya taifa, TBC1 kila Jumapili, kuanzia saa 3.00 hadi 3.30 usiku. 

"Aidha, tuko mbioni kuona namna vipindi hivyo vinavyoweza kurushwa kupitia vyombo vingine vya habari ili Watanzania wengi zaidi waweze kufahamu majukumu ya taasisi hii ya umma. Aidha, kwa zaidi ya miaka 8, Benki Kuu imekuwa ikiendesha semina kwa waandishi wa habari angalau mara moja kwa mwaka ili waweze kuielewa vizuri Benki Kuu na kupitia uelewa wao huo waweza kuuelimisha umma kuhusu kazi za Benki Kuu,"ameongeza.

Pamoja na mambo mengine, semina hiyo ya siku tano itaangazia mada mbalimbali ikiwemo kukuza uelewa kuhusu Dhamana za Serikali ili wananchi wengi zaidi waweze kushiriki katika uwekezaji huo.

Nyingine ni Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha, 2018 na Kanuni zake, Changamoto za Usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha ili kuisaidia taasisi kuwaelewesha Wadau utatuzi wa changamoto hizo.

Kufahamishwa maana ya Sera ya Fedha Safi katika mzunguko na nafasi ya wananchi katika kuifanikisha sera hiyo pamoja namna ya kutambua Alama za Usalama Katika Fedha za Tanzania na nyinginezo.

Nao washiriki wa semina hiyo wameonesha matarajio makubwa huku wakiahaidi baada ya mafunzo hayo watakwenda kutumia kalamu zao ipasavyo kwa ajili ya kuibuia fursa mbalimbali za kiuchumi ili ziweze kutumika katika kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news