NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa Mifuko ya Udhamini wa Mikopo ya Uuzaji Bidhaa Nje ya Nchi (Export Credit Guarantee Scheme – ECGS) na Miradi ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (Small and Medium Enterprises Guarantee Scheme – SME-CGS) imelenga kuondoa changamoto ya sharti la dhamana linalotolewa na benki nchini ili kutoa mikopo kwa wahitaji.
Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wauzaji Bidhaa nje ya Nchi (ECGS) ulianzishwa na Serikali mwaka 2002 kwa kutoa udhamini kwa wakopaji toka katika mabenki kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uuzaji bidhaa nje.
Aidha,Mfuko wa Udhamini wa mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME-CGS) hutoa udhamini kwa mabenki yaliyosajiliwa chini ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Benki Kuu kama wakala wa Serikali husimamia mifuko ya udhamini wa mikopo kwa njia ya mpito hadi hapo itakapoanzishwa taasisi inayojitegemea nje ya Benki Kuu.
Hayo yamesemwa leo Februari 15,2022 na Mchambuzi wa Masuala ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Fidelis Mkatte ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha.
Mafunzo ambayo yanaendelea katika Ukumbi wa Benki Kuu tawi la Mbeya yakiratibiwa na Benki Kuu ya Tanzania ambapo Bw. Mkatte alikuwa akiwasilisha mada iliyoangazia Majukumu ya Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania.
Amesema, Benki Kuu ilifikia hatua hiyo baada ya kuona kuna changamoto ya masharti ya kupata mikopo kutoka kwenye mabenki hasa inapokuja suala la dhamana.
"Hivyo tulianzisha Mfuko wa Dhamana ili kuondoa changamoto hiyo na kwakweli uamuzi huo umekuwa na manufaa makubwa,”amesema Mchambuzi huyo wa Masuala ya Fedha kutoka BoT.
Amesema, mfuko wa ECGS huwa unadhamini mikopo ya muda mfupi na muda mrefu. "Hudhamini asilimia 75 ya mkopo wa muda mfupi usiozidi mwaka mmoja, vile vile hudhamini asilimia 50 ya mkopo wa muda mrefu unaozidi mwaka mmoja.
"Mfuko huu umekuwa wa manufaa makubwa kwa wafanyabiashara na hata vyama vya ushirika na umewezesha mabenki kutoa mikopo mingi zaidi na ya muda mrefu,"amefafanua Bw. Mkatte.
Akieleza jinsi Mteja anavyoweza kunufaika na mifuko hiyo, Bw. Mkatte amesema kuwa, mteja akienda benki kuomba mkopo mfano mjasiriamali anayetaka kuanzisha mradi fulani na amekidhi vigezo karibu vyote vinavyohitajika isipokuwa dhamana, hapo ndipo Benki Kuu kupitia mfuko inapoingia ili aweze kukamilisha lengo lake akaanzishe biashara au mradi wake.
"Hivyo, benki husika hutoa taarifa kuhusu mteja huyo na Benki Kuu baada ya kujiridhisha basi hujazia kiasi cha fedha ambacho ni pungufu ya kile alicho nacho mteja na hivyo kuwa kama dhamana,”amesema Bw. Mkatte.
Akizungumzia kuhusu, Mfuko wa Udhamini wa mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME-CGS) amesema, mfuko huo ulianzishwa mwaka 2005 ukiwa na mtaji wa shilingi milioni mia tano ikiwa ni mchango toka serikalini.
"Udhamini hutolewa kwa mikopo ya kuanzia mwaka mmoja mpaka miaka mitano na udhamini hutolewa kwa miradi ya uzalishaji mali.
"Udhamini wa mikopo hutolewa kwa mikopo ya kuanzia shilingi milioni tano 5,000,000 hadi shilingi milioni 500,000,000,"amesema Bw.Mkatte.
Wakati huo huo, Bw. Mkatte amesema miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo kama Kurugenzi ni pamoja na ufinyu wa soko.
"Hii ni changamoto kubwa kwani sio wananchi wote wanaofikiwa na huduma za vyombo vya fedha na kutambua fursa kama hizi za kushiriki katika masoko fedha. Hali hii hufanya ukuaji wa soko kuwa wa taratibu sana.
"Changamoto nyingine ni mabadiliko ya hali ya uchumi na fedha duniani, kwani hali inapobadilika kama vile janga la UVIKO-19 linavyoendelea Duniani, matarajio ya uwekezaji wa fedha zetu kwa faida na pia kwa usalama yanakuwa na mashaka makubwa,"amefafanua Bw.Mkatte.