NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa,mchango wa wadau mbalimbali katika kuweka mazingira yenye kuwezesha uzalishaji na ukuzaji rasilimali ni hatua muhimu katika kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi nchini.
Dkt.Nicholaus Kessy ambaye ni Meneja Uchumi Tawi la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mkoa wa Mbeya ameyasema hayo leo Februari 14, 2022 wakati akiwasilisha mada kuhusu Utayarishaji na Utekelezaji wa Sera ya Fedha katika siku ya kwanza ya semina ya siku tano iliyoandaliwa na Benki Kuu kwa waandishi wa habari za biashara, uchumi na fedha katika Ukumbi wa Benki Kuu Tawi la Mbeya.
"Ukuaji endelevu wa uchumi unahitaji mazingira yenye utulivu wa bei na hivyo mchango wa sera ya fedha katika uchumi ni mkubwa na muhimu.Benki Kuu, inatekeleza sera zake kulingana na mwelekeo wa malengo mapana ya Serikali, na kwa uwiano na sera ya mapato na matumizi ya Serikali.
"Mafanikio katika kudumisha ustawi wa uchumi yanahitaji pia mchango wa wadau wengine katika kuweka mazingira yenye kuwezesha uzalishaji na ukuzaji wa rasilimali,"amefafanua Dkt.Kessy.
Amesema, ushiriki wa wadau ni muhumu kwa kuwa, pia Benki Kuu inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuhakikisha uchumi wa Taifa unaimarika.
"Benki Kuu nayo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi likiwemo lile la kutunga na kutekeleza sera ya fedha inayolenga utulivu wa bei.
"Pia kudumisha utulivu wa bei ikiwa ni hatua muhimu inayowezesha kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi nchini. Ni kwa sababu chanzo kikuu na cha kudumu cha mfumuko wa bei ni ongezeko la fedha lisilowiana na ongezeko la vitu halisi kwa maana ya bidhaa na huduma,"amefafanua Dkt.Kessy.
Amesema, Benki Kuu imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo kuhakikisha uwiano sahihi wa fedha na vitu halisi.
"Hii ni kwa sababu, Benki Kuu ya Tanzania ndiyo mtoaji pekee wa fedha kwa maana ya shilingi ya Tanzania hapa nchini, hivyo ina uwezo wa kuongeza au kupunguza ujazi wa fedha hapa nchini kupitia Sera ya fedha na utulivu wa bei,"amesema.
Utulivu wa bei
Dkt. Kessy anasema, utulivu wa bei huwa unapimwa kwa kuangalia mabadiliko ya fahirisi ya bei ya kapu la walaji au kwa maana nyingine mfumuko wa bei.
"Hivyo utulivu wa bei unahesabiwa kuwepo kama mfumuko wa bei sio wa juu au chini sana kwa kipindi kirefu,"anaeleza na kufafanua kuwa, utulivu wa bei ni muhimu zaidi nchi kwani unatoa majawabu kwa makundi mbalimbali wakiwemo wawekezaji.
Dkt. Kessy anasema, mfumuko wa bei unapokuwa mkubwa unasababisha wawekezaji kushindwa kufanya maamuzi hususani ya uwekezaji wa muda mrefu ambao una tija.
"Badala yake wanawekeza kwenye maeneo yanayohifadhi thamani kama vile kujenga nyumba, fedha za kigeni na biashara za muda mfupi kwa maana ya uchuuzi.
"Pia mfumuko wa bei unapokuwa mkubwa unasababisha mishahara kupoteza thamani haraka, hivyo wafanyakazi wanatafuta njia nyingine za kuongeza kipato na hivyo kupunguza tija, vivyo hivyo watu kupunguza kuweka amana za fedha kwa sababu thamani inamomonyoka haraka,"amebainisha Dkt.Kessy.
Wakati huo huo, Dkt.Kessy anafafanua kuwa, utulivu wa bei ni muhimu kwa sababu mfumuko wa bei unapokuwa mdogo sana au hasi unaondoa faida katika uwekezaji na hivyo kupunguza uzalishaji.
"Wazalishaji watatumia gharama kubwa zaidi katika kuzalisha kuliko kipato watakachopata na hivyo watapunguza au kuacha kuzalisha,"amesema.
Katika hatua nyingine, Benki Kuu ya Tanzania imewahakikishia wananchi kuwa, utulivu wa bei nchini umeendelea kusalia katika viwango vizuri kwani kulingana na vipimo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mataifa ya Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi, Tanzania ni ya pili ikitanguliwa na Rwanda.
Ni kwa kuwa na utulivu wa bei za vyakula ambapo hadi kufikia Desemba 2021 mfumuko wa bei kwa upande wa vyakula umebaki ndani ya lengo yaani kiwango cha asilimia 4.9 ya mfumuko wa bei ya chakula. Rwanda ikiwa ndiyo yenye mfumuko wa chini kabisa wa bei wa asilimia -2.1 katika kipindi cha Desemba 2021.
Aidha, Burundi ndiyo yenye mfumuko mkubwa wa bei unaofikia asilimia 10.0, huku ikifuatiwa na Kenya asilimia 9.1 na Uganda asilimia 5.3.