NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KAMPUNI ya michezo ya kubashiri ya Kimataifa, Betway Tanzania imezindua rasmi programu yake ya maboresho ya viwanja vya michezo.
Programu hiyo ambayo ni sehemu ya kampuni hiyo kurudisha kwa jamii inalenga kuchangia katika juhudi za maendeleo ya sekta ya michezo nchini.
Katika kutekeleza azma yake ya kuendeleza sekta ya michezo nchini Tanzania, kampuni ya Betway imeahidi kufanya mambo kadhaa ikiwemo kuchangia moja kwa moja katika maboresho ya miundombinu ya michezo, kuchangia vifaa na zana muhimu za michezo na kudhamini shughuli mbalimbali za michezo.
Kupitia programu hii ya maboresho ya viwanja vya michezo, Betway imepanga kuanza na viwanja vitano vya jijini Dar es Salaam.
Uwanja wa mchezo wa mpira wa kikapu wa Sea View uliopo Ocean Road, Ilala jijini Dar es Salaam ni wa kwanza kufanyiwa maboresho.
Uwanja huo ni moja ya viwanja vyenye historia kubwa katika mchezo wa mpira wa kikapu jijini Dar es Salaam na nchini Tanzania kwa ujumla, umefanyiwa maboresho makubwa yaliyohitajika kuurudisha katika hadhi ya viwanja vya mpira wa kikapu kitaifa.
Uzinduzi wa programu hiyo umeenda sambamba na bonanza la uzinduzi wa uwanja cha michezo wa mpira wa kikapu wa Sea View ambao ni uwanja cha kwanza kufanyia maboresho.
Katika uzinduzi huo wadau mbalimbali wa mchezo wa kikapu wamejumuika kwa kushindana na kuburudika huku wakifurahia mandhari mapya ya uwanja huo.
Akizungumza na wadau walioshiriki hafla ya uzinduzi na makabidhiano ya uwanja wa Sea View iliyofanyika Februari 5, 2022 jijini Dar es Salaam, Afisa Uendeshaji wa Betway Tanzania, Jimmy Masaoe ametaja maboresho yaliyofanyika katika uwanja huo ambao ni sehemu ya kituo cha michezo cha Gymkhana.
“Kama sehemu ya kuimarisha miundombinu ya michezo na kuwafanya watanzania kuipenda na kufurahia michezo tumefanya maboresho makubwa ya uwanja huu ikiwemo maboresho ya majukwaa, eneo la kuchezea, magoli, na taa kwa ajili ya matumizi ya usiku.
"Maboresho haya yataongeza hadhi ya uwanja huu wenye historia kubwa katika mchezo wa mpira wa kikapu lakini pia utavutia wachezaji wengi wa mpira wa kikapu kufanya mazoezi na kufanya mashindano,"amesema Masaoe.
Akifafanua kuhusu muendelezo wa program hiyo, Masaoe aliweka wazi kuwa uzinduzi wa maboresho hayo ni mwanzo wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya maboresho ambayo inatarajiwa kuendelea katika mikoa mingine ya Tanzania.
“Uzinduzi wa leo ni mwanzo wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya maboresho ya viwanja vitano katika jiji la Dar es Salaam.
"Maboresho hayo yamelenga viwanja ambavyo vina matumizi makubwa katika mchezo husika ili kutoa nafasi kwa wanamichezo na mamlaka kuwa na miundombinu yenye hadhi ya kuendesha shughuli za michezo. Tunawasihi wanamichezo na mamlaka za usimamizi kusimamia vyema miundombinu hii ili iweze kuleta tija inayotarajiwa kwenye michezo kwa muda mrefu,"amesisitiza Masaoe.
Kwa upande wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Mwenze Fiston ametoa shukurani kwa kampuni ya Betway kwa kuja na programu ya maboresho ya uwanja ambayo imeifaidisha tasnia ya mchezo wa mpira wa kikapu. Fiston aliongeza kwamba wataendelea kuhirikiana na Betway na wadau wengine kukuza mchezo wa mpira wa kikapu nchini Tanzania ili kuongeza ajira kwa watanzania wengi zaidi kupitia mchezo huo.
“Ni furaha kubwa kwetu kuona Betway ambayo ni kampuni kubwa ya michezo duniani imeona na kutambua umuhimu wa mchezo wa mpira wa kikapu hapa nchini na kuamua kuelekeza nguvu katika kuboresha miundombinu ya michezo hiyo. Tumepokea kwa furaha sana program hii na tunaamini haitashia hapa bali itaendelea na mikoa mingine. TBF tunawaahidi kushirikiana na mamlaka nyingine kama Shirikisho la Mpira wa Kikapu jijini Dar es Salaam na Serikali katika kutunza miundombinu ambayo imeboreshwa na Betway ili iweze kusaidia michezo kwa muda mrefu zaidi,"alisema Fiston.
Katika bonanza la uzinduzi michezo mitatu ilichezwa ikiwemo mchezo wa maveterani wa wa mpira wa kikapu wa jiji la Dar es Salaam, mchezo kati ya Dream Team na Dar City kwa upande wa wanawake huku Dar es Salaam All Stars wakichuana na Pwani All Stars kwa upande wa wanaume. Wachezaji na mashabiki wa mpira wa kikapu wameonesha furaha yao kufuatia maboresho ya uwanja huo.
Tags
Michezo