NA FRESHA KINASA
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga, amesema kuwa, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma unapaswa kukamilika haraka ili uanze kuleta tija kwa wananchi wa Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla hatua ambayo pia itawezesha kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni kiongozi bora na wa mfano kwa Taifa na Afrika.
Amesema kuwa, Wilaya ya Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla una historia kubwa na ya kipekee kwa kumtoa kiongozi mahiri, shupavu na jasiri aliyeleta Uhuru na ukombozi wa nchi nyingine za Afrika, hivyo uwanja wa ndege lazima upanuliwe haraka kusudi uchochee ukuaji wa kiuchumi ikiwemo kupokea wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi watakaokuja kutalii Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kuongeza mapato.
Ameyasema hayo leo Februari 2, 2022 wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Musoma Mjini iliyojumuisha pia Mabalozi wa mashina wa Wilaya ya Musoma Mjini na wazee wa mabaraza katika kikao kilichofanyika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mara uliopo Mjini Musoma.
Mbali na hayo, amewataka watendaji wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa weledi kwa kusimamia masilahi ya wananchi na kutatua kero mbalimbali kutokana na dhamana waliyopewa. Huku pia akisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kimebeba dhamana ya maisha ya Watanzania hivyo kitaendelea kuhakikisha maisha ya Watanzania yanazidi kuwa mazuri sambamba na kuimarisha umoja, mshikamano uliopo.
Pia, amesema Chama Cha Mapinduzi kinatambua kwa dhati mchango mkubwa unaofanywa na Mabalozi wa mashina maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kuimarisha uhai wa chama na utatuzi wa migogoro hivyo chama kitazidi kushirikiana nao kwa karibu.
"Leo nchi ya Kongo wanamlilia Patrick Lumumba hawawezi kumpata, Libya wanamlilia Ghadafi hawawezi kumpata. Niwaombe Mabalozi muendelee kusimamia amani na umoja uliopo katika maeneo yenu na Watanzania wote tuzidi kudumisha amani na umoja.Tuendeleeni kumuunga mkono Rais Samia aendelee kuleta maendeleo katika taifa letu, tuzidi kumuombea mchana na usiku ni kiongozi ambaye ataifikisha nchi yetu panapotakiwa sote tunataka kasi aliyonayo,"amesema Kanali Mstaafu Lubinga.
Katika hatua nyingine, Kanali Mstaafu Lubinga amewataka wana CCM kutofanya makosa katika uchaguzi wa viongozi mbalimbali ndani ya chama hicho ambapo amesema wana CCM wanawajibu wa kuchagua viongozi waadilifu wasiopenda rushwa, ufisadi, na pia wenye tabia njema na wawajibikaji kwa masilahi mapana ya chama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Mjini, Benedictor Magiri amesema maadhimisho hayo ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM yatakayofanyika Musoma tarehe 5/2/2022 ni heshima kubwa kwa wakazi wa Musoma na Mkoa wa Mara ambapo amewaomba wana CCM na wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku hiyo ikiwemo kushiriki matembezi ya mshikamano na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
"Wana Mara wana Musoma Mheshimiwa Rais ametuheshimisha sana. Twendeni kwa wingi mapema sana siku hiyo tukaungane kwa pamoja kumsikiliza Mwenyekiti na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 5/2/2022," amesema Magiri.
Pia, Magiri amesema mwaka huu ni wa Sensa hivyo amewaomba wananchi na wana CCM wote wa Musoma kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la Sensa ili wahesabiwe kwa manufaa yao na manufaa ya Taifa pia.
Aidha,Kanali Mstaafu Lubinga ametembelea upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma, madarasa katika Shule ya Sekondari Nyamitwebiri pamoja na Kituo cha Afya Rwamulimi katika Manispaa ya Musoma.
Tags
Habari