NA MWANDISHI MAALUM
CHUO cha Taifa cha Utalii kimezindua mafunzo ya siku tano ya UVIKO-19 kwa wadau zaidi ya 140 waliopo kwenye mnyororo wa huduma za utalii katika Mkoa wa Ruvuma ili kuwajengea uwezo wa namna ya kujikinga katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo wakati wanapotoa huduma kwa wageni pindi wanapotembelea maeneo yao.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Shogo Mlozi akizugumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya UVIKO-19 kwa wadau wa Sekta ya Utalii yaliyofanyika Februari 21,2022 Katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Manispaa Mji wa Songea.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika Februari 21,2022 katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Mji wa Songea, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Shogo Mlozi Sedoyeka amesema kuwa, mafunzo hao yamefadhiliwa na MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAKABILIANO DHIDI YA UVIKO-19 kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dkt. Sedoyeka amesema kuwa, chuo kimeamua kutoa mafunzo hayo kwa wadau wa utoaji wa huduma za utalii baada ya kubaini kuwa baadhi yao walikuwa bado hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na UVIKO-19 pindi wanapowahudumia watalii.Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Steven Ndaki akizungumza alipokuwa akifungua rasmi mafunzo hayo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
Amesema kuwa, chuo kinatoa mafunzo hayo kwa wadau muhimu katika mnyororo wa utalii ili wadau hao waweze kuboresha huduma zao na thamani ya pesa inayotolewa na mgeni au mtalii kuonekana.
Pia amesema, chuo kinatoa mafunzo hayo kwa watoa huduma hao kwa kuwa wengi wao hawana weledi wa utoaji huduma hasa wakati huu wa janga la UVIKO-19 ili kujikinga wao wenyewe pamoja na wageni wanaopata huduma zao.
Aidha, Dkt. Sedoyeka amesema, mafunzo haya kwa mkoa wa Ruvuma yamekuja wakati sahihi ambapo kuna shughuli mbalimbali za utalii wa makumbusho, kupanda milima, fukwe na nyinginezo lakini watoa huduma kutokuwa na uelewa mpana na wa kibunifu wa kutoa huduma hizo.
Pia amesema, mafunzo yanatolewa katika mikoa nane ikijumuisha Lindi, Mtwara, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Mara na Mwanza ambapo mpaka sasa mafunzo yamekamilika mkoa wa Lindi na Mtwara na yanaendelea mkoa wa Ruvuma na Njombe kwa siku tano,na badaae kufikia mikoa mingine minne.
Dkt. Naiman Mbise, Mratibu wa Mradi wa Mradi Mafunzo kwa watoa huduma katika mnyororo wa Sekta ya Utalii nchini chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 akizungumza wakati wa ufunguzi huo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Sedoyeka amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo ambazo zinawezesha kukabiliana na UVIKO-19 kwenye jamii pamoja na kwamba mpango huo unaOnesha nia madhubiti ya Serikali ya Awamu ya Sita Katika kukabiliana na janga hilo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Steven Ndaki ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa huo, Brigedia Wilbert Ibuge kwenye uzinduzi huo katika nafasi ya mgeni rasmi amesema kuwa, sekta ya utalii imekuwa ikitoa fursa mbalimbali ikiwemo suala la ajira hivyo inatakiwa kuizingatia kikamilifu.
Ndaki amesema kuwa, katika kipindi cha janga kubwa la Corona, utalii uliyumba katika nchi mbalimbali hivyo kwa sasa inatakiwa kuitumia elimu ya UVIKO-19 ipasavyo ili kulinda watalii na jamii kwa ujumla.
Mratibu wa Mafunzo hayo Mkoa wa Ruvuma, Elina Makanja akizumguzia jinsi walivyojipanga katika kutoa mafunzo hayo mkoani humo.
Naye Maajabu Mbogo ambaye ni Afisa Utalii katika Pori la Limbaramba ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo amesema kuwa, mafunzo hayo yataleta neema ya kuongezeka kwa watalii na kuifanya Serikali iweze kupata mapato kupitia watalii hao.
Mbogo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka fedha za UVIKO-19 katika sekta hiyo na kwamba Rais ameangalia maslahi mapana ya nchi hasa katika kuikomboa Sekta ya Utalii nchini ambayo imeathirika na janga hilo kwa kiasi kikubwa.
Wadau mbalimbali wa Sekta ya Utalii Mkoa wa Ruvuma wakifuatilia hotuba mbalimbali za ufunguzi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Shogo Mlozi (wa kwanza kushoto aliyekaa), Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Steven Ndaki (katikati) na Mratibu wa Mafunzo hayo Mkoa wa Ruvuma, Elina Makanja wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Taifa cha Utalii.
Katika mafunzo hayo jumla ya mada sita zitatolewa na wakufunzi mbalimbali kutoka Chuo cha Taifa cha Utalii na mafunzo hayo yatafikia kilele chake Februari 25,2022.