NA ROTARY HAULE
CHAMA cha Walimu (CWT) kimewapiga jeki walimu wa Shule ya Msingi Jitihada iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa kuchangia kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajili ya kutatua changamoto ya ukosefu wa viti iliyokuwa ikiwakabili walimu hao kwa muda mrefu.
Fedha hizo zimekabidhiwa Februari 18,2022 shuleni hapo na Mwekahazina wa CWT Taifa, Abubakar Allawi kwa Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, John Mihayo halfa ambayo ilishuhudiwa na walimu wa shule hiyo pamoja na uongozi wa CWT ngazi ya mkoa na wilaya.
Aidha,miongoni mwa viongozi alioambatana nao Allawi ni Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Mwajuma Mgonze,Katibu wa CWT Wilaya ya Kibaha, John Kigongo, Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Kibaha, Mwita Magige na wajumbe wengine.
Akizungumza na walimu wa shule hiyo Allawi,amesema kuwa CWT inatambua juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya shule kwa kujenga madarasa kila wilaya.
Amesema,ujenzi wa madarasa hayo ni mkombozi wa wanafunzi wa Tanzania na kwamba ni lazima kwa pamoja waendelee kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake kubwa alizofanya katika sekta ya elimu.
Allawi amesema,kama Serikali imefanya kwa kiwango hicho na CWT lazima iunge mkono kwa kushiriki katika kutatua changamoto ndogondogo za walimu zilizopo katika shule zao.
"CWT inatambua changamoto za walimu wa shule hii ikiwemo ya kukosa viti vya kukalia na tulipopata taarifa hii tuliahidi kuja kuchangia kiasi cha shilingi milioni moja na leo tumekuja kutekeleza ahadi yetu,"amesema Allawi.
Allawi amesema, mchango huo ni sehemu endelevu ya kazi zinazofanywa na CWT na ana imani kiasi hicho cha fedha kitasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa viti shuleni hapo huku akiahidi kuendelea kuwasaidia walimu hao kwa mahitaji mengine.
"Tumekuja shuleni hapa kwakuwa tunatambua kuna wanachama wa CWT kwa asilimia 90 na tumekuja kuwatembelea na kutatua changamoto yenu ya ukosefu wa viti vya kukalia walimu ofisini na tunatoa hii milioni moja kwa ajili ya kununulia viti,"amesema Allawi.
Kwa upande wake Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Mwajuma Mgonze amesema kuwa, utambuzi wa mtu uanza na nafsi yake ambapo amemshukuru mwekahazina wa Taifa kwa kazi kubwa na nzuri aliyofanya.
Mgonze,amesema juhudi alizozifanya Allawi katika kusaidia kutatua changamoto ya walimu hao amekivika nguo chama na viongozi wa CWT Mkoa wa Pwani na hata wilaya .
Aidha,Mgonze amesema CWT ipo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wanachama wake ambapo amewataka walimu hao kuendelea kuwa na imani na chama chao kwa kuwa kazi inayofanyika inaleta maslahi chanya kwa wote.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, John Mihayo amekishukuru chama hicho kupitia mwalimu Allawi na kusema fedha waliyotoa itasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa viti vya walimu shuleni.
Hata hivyo,Mihayo amemuomba Allawi kuendelea kusaidia shule hiyo katika changamoto nyingine zilizopo ili kuhakikisha wanachama wao wanafanya kazi katika mazingira mazuri zaidi.