Dar, Zanzibar waongoza kuwa na noti safi,wenye noti zilizochakaa watajwa

NA GODFREY NNKO

MSIMAMIZI wa Mzunguko wa Sarafu kutoka Idara ya Sarafu chini ya Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw.Ilulu Said Ilulu amesema kuwa,Zanzibar na Dar es Salaam wanaongoza kwa kuwa na noti safi huku Mbeya, Dodoma, Mwanza, Iringa, Kagera (Bukoba), Kigoma wakiongoza kwa kuwa na noti zilizochakaa.
Pia kwa uchache mikoa inayohudumiwa na Benki Kuu tawi la Mtwara na lile la Arusha wanatajwa kutunza vizuri fedha hizo ingawa kuna baadhi wanashindwa kufanya hivyo.

Hali hiyo imetajwa inachangiwa na namna ambavyo wananchi wamekuwa wakihifadhi fedha hizo na matumizi yao ya kila siku,jambo ambalo kwa namna moja au nyingine linaiongezea Serikali gharama ya kuchapisha fedha mpya.
"Acheni kufunga fedha kwenye nguo, tunzeni fedha kwenye benki siyo kwenye mashimo au magunia. Kwa sababu kutokana na aina ya uhifadhi, noti unakuta imechakaa sana, tena kabla ya kufikia muda wake wa matumizi katika mzunguko, inatulazimu sasa (BoT) tuingie gharama kubwa kwa ajili ya kuzikusanya, kuziteketeza na kuanza hatua ya kuchapisha noti mpya.

"Gharama zinazotumika kuchapisha fedha hizo wakati mwingine zingeelekezwa katika mipango ya Serikali maana ni kubwa sana ili kutekeleza miradi ya maendeleo. Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunazihifadhi vizuri fedha zetu ili ziweze kudumu zikiwa safi katika mzunguko;
Bw.Ilulu ameyasema hayo leo Februari 17, 2022 ikiwa ni siku ya nne ya mafunzo kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara yanayoendelea katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mbeya.

Mafunzo hayo ya siku tano yanaratibiwa na Benki Kuu ambapo Bw.Ilulu alimeyabainisha hayo baada ya waandishi kufanya ziara na kujionea namna ambavyo fedha zinavyokusanywa na kuchambuliwa ili kuweza kuainisha zile safi kwa ajili ya kurudisha katika mzunguko na zile ambazo zimechakaa kwa ajili ya kuziteketeza.
Bw. Ilulu anasema kuwa, wameyabaini hayo kutokana na namna ambavyo benki za biashara zinavyorudisha noti nyingi chakavu katika matawi ya Benki Kuu katika Kanda za Kati, ya Ziwa na Kanda ya Nyanda za Juu na Kaskazini.

Benki Kuu ya Tanzania licha ya kuwa na makao makuu jijini Dodoma pia ina makao makuu madogo mawili ikiwemo Zanzibar na Dar es Salaam huku ikiwa na tawi mkoani Mbeya,Mwanza, Arusha na Mtwara ambayo yamekuwa yakitoa huduma kwa mikoa husika na ile ya jirani.

Msimamizi huyo amesema kuwa, ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anahifadhi fedha katika mazingira mazuri hususani kuziweka benki ili ziendelee kuwa katika mzunguko.

Bw. Ilulu amesema, Benki Kuu inataka sarafu safi pekee zitumike nchini na kwamba noti ikichakaa kwa asilimia 50 inaweza kurudishwa benki ili kubadilishwa.

Pia amesema, ni jambo jema kwa kila mwananchi kujiunga na huduma za benki nchini, kwani ukiwa na akaunti, siku ikatokea ukawa na fedha zilizochaa itakuwia rahisi kuzipeleka benki waweze kukubadilishia kwa ajili ya kuzirejesha Benki Kuu.
"Na mtu yeyote hana ruhusa ya kuharibu au kuteketeza fedha za Tanzania, ukiona imechakaa zipelekee katika benki za biashara, ukiwa na akaunti huko itakuwia rahisi kubadilishiwa, wakishakubadilishia, watatuletea nasi (Benki Kuu) baada ya kuzichambua na kubaini hazifai tena kurejea kwenye mzunguko tutatumia mfumo wetu kuziteketeza.

"Fedha hizo zinarejeshwa Benki Kuu ili tuweze kupata picha kamili ya fedha ambazo hazipo katika mzunguko ikizingatiwa kila noti ina namba zake za siri ambazo hazijirudii, ikitoka imetoka na mwenye mamlaka pekee ya kuteketeza fedha chakavu ni Benki Kuu ya Tanzania na si mtu mwingine yeyote,"amesema Bw.Ilulu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news