NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Mariam Ditopile amesema, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya muda mfupi madarakani anazidi kuwaumbua wale wote waliombeza kuhusu uendelezaji wa miradi ya kimkakati Jiji la Dodoma iliyoasisiwa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Mbunge Ditopile ameyasema hayo leo Februari 9,2022 baada ya hafla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuweka Jiwe la Msingi mradi wa Ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje katika mji wa Dodoma, Barabara hiyo itatoka Ihumwa-Matumbulu-Nala-Veyula-Ihumwa Kilomita 112.3.
Hafla hiyo imefanyika kwenye Sherehe zilizofanyika leo tarehe 09 Februari, 2022 katika eneo la Veyula jijini Dodoma
"Nampongeza kidhati Rais Samia kwa kuendelea kutimiza ahadi zake kwa vitendo za kuendeleza miradi yote ya kimkakati iliyoasisiwa na Hayati Dkt. John Magufuli Jijini Dodoma, wote ni mashahidi miradi inaendelezwa kwa kasi kubwa sana.
"Yalikuwepo maneno kwamba Hayati ameondoka na miradi itasimama au haitafanyika, lakini sasa ni tofauti, miradi yote inaendelezwa. Mradi huu wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma ni mradi ulisubiriwa kwa Hamu na wana Dodoma utalibadilisha hili jiji letu.
"Mradi mwingine unaendelezwa na Rais Samia jijini Dodoma ni ujenzi wa Hospitali Mpya ya Jiji la Dodoma na tayari Rais Samia ametoa zaidi ya Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wake kuanza, sisi wana Dodoma tunamshukuru na kumpongeza Sana.
"Rais Samia anaonyesha kwa vitendo anayo nia ya dhati ya kuendeleza miradi yote ya mtangulizi wake, nawasihi watanzania tupuuze maneno ya watu wachache wasioitakia mema Nchi yetu, Rais Samia atatekeleza miradi yote aliachiwa tena kwa kasi kubwa na ufanisi,"amesema na kutaja baadhi ya miradi kuwa ni;
-Njia ya mchepuko Kusini mwa Jiji la Arusha 42.4KM
- Barabara ya Mbinga-Mbamba Bay 66KM
-Barabara ya Singida-Babati-Minjingu 223.5KM
- Barabara ya Arusha-Namanga 105KM
- Iringa- Dodoma 260KM
- Namtumbo-Tunduru 190KM
- Mayamaya-Bonga 188KM
"Tunduru - Mangaka Mtambaswala 202.5KM yote inaendelea kutekelezwa na itakamilika kwa wakati, huyu ndo Rais Samia wa Vitendo sio Maneno,"amesema Mheshimiwa Ditopile.
Tags
Habari