NA FRESHA KINASA
BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) Mkoa wa Mara linaendesha zoezi la utoaji wa elimu katika Manispaa ya Musoma imhusuyo mtumiaji wa huduma za maji na nishati juu ya haki na wajibu wao katika kuwajengea uelewa wa masuala mbalimbali waweze kuyatambua katika kuimarisha ufanisi wa ubora wa huduma.
Katibu wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji nchini, Mhandisi Goodluck Mmari akisaini kitabu alipowasili katika banda la EWURA CCC lililokuwa katika soko la Nyamatare ambapo zoezi la utoaji wa elimu imhusuyo mtumiji wa Huduma za Nishati na Maji limefanyika. Aliyesimama katikati ni Katibu wa Kamati za Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji Mkoa wa Mara, Martine Mlalahasi na pembeni yake ni mwananchi aliyefika kupewa elimu.
Katibu wa Kamati ya Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na (EWURA ) Mkoa wa Mara. Martine Mlalahasi akizungumzia zoezi hilo lililoanza Februari 22, 2022 katika soko la Nyamatare Manispaa ya Musoma wakati akitoa elimu kwa wananchi waliofika banda la EWURA CCC amesema, watumiaji wa huduma wana wajibu wa kutambua wajibu wao pamoja na haki, hatua ambayo itawafanya wafurahie huduma na kuweza kushiriki kikamilifu kutunza miundombinu kwa manufaa endelevu.
Katibu wa Kamati ya Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na EWURA mkoani Mara,Martine Mlalahasi.
Amesema, baadhi ya wananchi hawana ufahamu wa mambo mbalimbali kuhusiana na huduma na wakati mwingine wanapokuwa na kero hawajui taratibu za kufuata na wapi wapeleke malalamiko yao, lakini wakielimishwa kikamilifu watatambua vyema wajibu wao ikiwemo matumizi halali ya huduma na kupata njia sahihi za kupeleka kero zao badala ya kunung'unikia huduma bila ufumbuzi thabiti.
"Wananchi tunawaelimisha watambue wajibu wao mathalani, kulipia ankara zao kwa wakati baada ya kutumia huduma, kutunza miundombinu ya huduma ili iwe endelevu wanapoona katika maeneo yao kuna dosari watoe taarifa wahusika wafanye marekebisho badala ya kukaa kimya. Na pia wana wajibu wa kulalamikia huduma mbovu ama isiyokidhi viwango na katika hili lazima malalamiko yafuate utaratibu wa kuwasilisha na kushughulikia kama ulivyowekwa na mdhibiti," amesema Martine.
Pia, amesema mtumiaji ana haki ya kuelimishwa kuhusu huduma zitolewazo ili kumpa maarifa na ujuzi wa kumwezesha kuchagua huduma stahiki ikiwemo sera, miongozo na kanuni mbalinbali, elimu ya utatuzi wa migogoro baina ya mtoa huduma na mteja, viwango vya ubora pamoja na mkataba wa huduma kwa mteja.
"Pia mtumiaji ana haki ya kufidiwa kutokana na kupatiwa bidhaa zenye dosari ama huduma mbovu, na pia ana haki ya kupata utatuzi mzuri wa madai yake kama hasara imetokana na mtoa huduma na madai yote ya fidia lazima yazingatie kanuni na taratibu zilizopo sambamba na kuweza kuchunguza huduma kwa kuzingatia bei na ubora," amesema Martine.
Neema Jackson ni mkazi wa Kata ya Nyamatare Manispaa ya Musoma aliyefika kuelimishwa katika Banda la EWURA CCC amesema, awali hakutambua kwamba anaweza kulalamikia huduma iwapo haikidhi kiwango stahiki kwa kuhofia kufikishwa mahakamani, lakini baada ya elimu aliyopatiwa amepata ujasiri na ufahamu wa kutosha.
"Wakati mwingine nimekuwa nikiwaza kwamba nikilalamikia huduma naweza kushitakiwa naikwamisha Serikali kukusanya kodi kumbe kulalamikia huduma mbovu ni haki yangu? Elimu hii kweli imenifungua macho kabisa," amesema Neema.
Naomi Marwa ni mkazi wa Nyamatare amesema, atakuwa balozi kwa wengine ambao hawakupata fursa ya kufika katika banda hilo kwa kuwaelimisha umuhimu ya kulipia ankara za matumizi ya huduma kwa wakati kwani kunawezesha miradi kujiendesha kwa faida ya wananchi wote kutokana na fedha zinazokusanywa kutoka kwa wateja ikiwemo ankara za maji.
Awali Mwenyekiti wa EWURA CCC Mkoa wa Mara, Robinson Wangaso amesema kuwa, elimu hiyo ina faida kubwa kwa wananchi kwani inawafikia mahala walipo katika maeneo yao na kuwapa uwanda mpana wa kuuliza maswali na kupatiwa majibu pamoja na vitini vya kujisomea.
Ambapo elimu hiyo imeanza kutolewa katika Kata ya Nyamatare sokoni Februari 22, 2022, Februari 23, 2022 itatolewa Nyakato kwa Saanane, Februari 24 itatolewa Bweri Stendi na Februari 25, 2022 Nyasho Sokoni ambapo amewahimiza wananchi kujitokeza kupata elimu hiyo ya bure.