NA FRESHA KINASA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA) imewataka wananchi kutumia mafundi wenye weledi, ujuzi na leseni wanapohitaji huduma za kuunganishiwa umeme katika nyumba na makazi yao, hatua ambayo itasaidia kuondokana na majanga mbalimbali yanayopelekea kupoteza mali zao na kuhatarisha maisha.
Kauli hiyo imetolewa Februari 16, 2022 na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa,George Mhina wakati akizungumza katika semina iliyowakutanisha mafundi umeme, wahandisi na taasisi mbalimbali zinazohisiana na sekta ya umeme.
Semina ambayo inafanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Mwembeni Complex Manispaa ya Musoma mkoani Mara ili kuwajengea uwezo mafundi umeme, wahandisi na taasisi mbalimbali zinazohisiana na umeme katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhina amesema kuwa, wananchi wanawajibu wa kutumia mafundi waliosoma na kupewa leseni katika huduma zao ili kuendana na ubora wa huduma pamoja na usalama wa mali zao na maisha yao badala ya kutumia mafundi vishoka wasio na weledi, ubora na leseni kwa mujibu wa sheria.
"Majanga yamekuwa yakitokea mara kwa Mara ikiwemo nyumba kuungua, shule lakini uchunguzi unapofanyika unakuta vifaa vilivyotumika havina ubora ama mafundi waliohusika hawana vigezo kwa mujibu wa sheria. Niwaombe Watanzania kutumia mafundi ambao wamekidhi vigezo vyote vya kutoa huduma bora na TANESCO pia watumie mafundi ambao wamekidhi viwango kuwezesha usalama wa mali za watu na maisha,"amesema Mhina.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Ally Hapi akifungua semina hiyo amesema kuwa, Utambuzi wa Mafundi wenye Leseni ni Muhimu sana kuendana na matakwa ya kisheria ambapo ameitaka EWURA kuwasajili mafundi wasio na leseni ambao wamesoma kusudi wapate leseni wafanye kazi zao kwa uhuru, ubora na kwa kiwango stahiki.
"Vijijini Umeme sio anasa imekuwa huduma ya lazima kwa maendeleo ya huduma mbalimbali kujenga uchumi wao. Jambo la ajabu wapo mafundi wasio na weledi, lakini wanatoa huduma maeneo mbalimbali hii ni hatari, takwimu zinaonesha kwamba katika kanda ya ziwa tuna mafundi 374 tu wenye leseni mkakati unahitajika kuongeza mafundi wenye leseni watakaokidhi viwango.
"Vyuo vya ufundi vina kazi ya kufundisha vijana na wale waliosoma wahamasishwe wapate leseni, tunakwenda kwenye utambuzi wa anuani za makazi, tutumie anuani hizi kutambua pia mafundi wa umeme wenye leseni wako katika maeneneo gani, kitongoji gani, ambao wamethibitishwa na EWURA, tuwapunguzie tabu wananchi kuingia kwenye mtego wa vishoka. Ufundi ni sayansi lazima wasome,"amesema Hapi.
"Vyuo pia vifanye mawasiliano na mamlaka husika zitengeneze mazingira bora ya kushirikiana kwa Karibu ili mwanafunzi anapokuwa chuoni awe na uhakika wa leseni baada ya kuhitimu. Vyuo vya Kati ni Muhimu sana kuleta mabadiliko katika jamii vijana wapikwe vyema katika vyuo hivyo ikiwemo VETA na NACTE,"amesema.
Kwa upande wake, Idi Bugingo ambaye ni fundi wa umeme anayeshiriki semina hiyo, amesema kuwa, mafundi wenye leseni Mkoa wa Mara wameanzisha umoja wao kwa lengo la kuisaidia Serikali kuwa na mafundi bora wenye weledi kuendana na mahitaji ya utoaji wa huduma bora.
Na amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi kusaidia mafundi wenye leseni kutekeleza miradi mbalimbali ya kuunganisha umeme katika majengo ya Serikali, ombi ambalo limepokelewa.
Semina hiyo imelenga kuwapa uelewa washiriki wote wa semina hiyo kutekeleza majukumu yao kwa ubora na weledi ambapo mambo mbalimbali yanayowahusu wataelimishwa.