Awali Balozi wa Italia nchini Tanzania, Marco Lombardi alimueleza Rais Dkt. Mwinyi kwamba Serikali ya Italia inaziona juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivyo, iko tayari kuendelea kuziunga mkono.
Balozi Lombardi amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba Italia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika hapa nchini.
Katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Balozi Lombardi alimueleza Rais Dkt.Mwinyi azma ya ubalozi huo kufanya kongamano kubwa la biashara mwezi Septemba mwaka huu 2022 hapa Zanzibar ili kujadili fursa mbalimbali za uchumi zilizopo.
Aidha, alimueleza Rais Dkt.Mwinyi azma ya kampuni kubwa za nchi hiyo kufanya safari zake za ndege moja kwa moja na sio zile za msimu kama ilivyo kwa hivi sasa hatua ambayo itaimarisha zaidi sekta ya utalii na biashara.
Sambamba na hayo, Balozi huyo wa Italia alimueleza Rais Dkt. Mwinyi mikakati iliyoiweka katika kuanzisha vyuo vya ufundi hapa hapa Zanzibar ambavyo, pamoja na mambo mengine, vitasaidia katika kuimarisha sekta ya utalii.
Balozi Lombardi alimuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba Serikali yake itaiunga mkono Sera ya Uchumi wa Buluu ili kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua na kufikia malengo iliyojiwekea.