NA MWANDISHI MAALUM-WUU
NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameiagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kukamilisha kazi za ujenzi wa jengo la mama na mtoto na kukabidhi jengo hilo kwa Wizara ya Afya ifikapo Machi 20, 2022 ili kuboresha huduma ya afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza-Sekou Toure.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachuzibwa wakati akitoka kukagua ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Sekou Toure linalotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoani Mwanza.
Mhandisi Kasekenya ameyasema hayo mkoani Mwanza wakati akikagua maendeleo ya utekelezaji wa jengo hilo ambao umefikia asilimia 94 ya kazi zote na kuridhishwa na kasi ya ujenzi na ubora wa jengo hilo.
“Hakikisheni inapofika tarehe hiyo muwe mmekamilisha kazi zote na kukabidhi Wizara ya Afya ili Wizara wahamishie huduma na wagonjwa katika jengo hili na kuruhusu ujenzi wa majengo mengine katika hospitali hii kuendelea,”amesisitiza Kasekenya.
Mhandisi Kasekenya ameipongeza TBA kwa kutekeleza mradi huo wenye sakafu sita kwa mfumo wa buni-jenga na kukamilisha kwa viwango vya ubora unaoendana na thamani ya fedha ya mradi.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoa wa Mwanza Mhandisi Moses Urio, alipokuwa akikagua ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Sekou Toure linalotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mkoani Mwanza.
Aidha, amewataka pia wateja wa wakala huo kulipa kwa wakati pindi wakala unapotekeleza miradi yao ili kutokwamisha utelezaji wa miradi mingine na miradi kuchukua muda mrefu kukamilika.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa mradi wa jengo hilo utakapomilika utaboresha huduma ya afya kwa wananchi hususani akina mama na watoto wa Mwanza na mikoa jirani, msongamano kwa wagonjwa uliopo sasa ambapo jengo litakuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa vitanda 261 na pia utapunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua kwa kiasi kikubwa.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Moses Urio, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, wakati alipokagua maendeleo yaliyofikiwa ya ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa – Sekou Toure linalotekelezwa na Wakala huo, mkoani humo.
Naye Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Mwanza, Mhandisi Moses Urio ameahidi kukamilisha kazi zilizobaki za ujenzi mapema iwezekanavyo na kukabidhi kwa muda uliopangwa na kwa kwa kuzingatia ubora.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachuzibwa, amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa maandalizi yapo tayari kwa ajili ya kuhamisha huduma katika jengo hilo jipya watakalokabidhiwa na hivyo kusaidia kuendelea na maboresho ya majengo mengine mapya katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Sekou Toure.
Muonekano wa nje ya jengo jipya la Mama na Mtoto katika Hospital ya Rufaa ya Mkoa – Sekou Toure linalojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao ujenzi wake umefikia asilimia 94. Jengo hilo linagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 10.1 na kutarajiwa kuanza kutumia mwezi Machi, 2022. (PICHA NA WUU).
Jengo la Mama na Mtoto likikamilika litakuwa na jumla ya vitanda 261, vyumba viwili vya upasuaji, vyumba vya matazamio baada ya upasuaji, vyumba vya kujifungulia, wodi za watoto chini ya mwezi mmoja na chini ya umri wa miaka mitano, vyumba vya madaktari, vyumba vya kubadilishia nguo, ofisi za viongozi na mapokezi.