NA ROTARY HAULE
WAJUMBE wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Pwani wameazimia kuanza kufanya kongamano kubwa la kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuepushwa na shari katika utekelezaji wa majukumu yake.
Maamuzi hayo yametolewa katika kikao chao na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge kilichoketi Mjini Kibaha kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ikiwemo la Rais Samia.
Shehe Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Hamisi Mtupa amesema kuwa, Rais Samia anafanya kazi kubwa ya kuliongoza Taifa sambamba na kuhakikisha analeta ustawi wa jamii kwa kuboresha huduma mbalimbali.
Mtupa amesema kuwa, kazi ya Urais ni ngumu na hivyo inahitaji makanisa na misikiti kutanguliza maombi juu ya kumuombea Rais ili aweze kuendelea vyema kutimiza malengo yake.
Amesema kuwa,Machi 19 mwaka huu Rais Samia atatimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani, lakini amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yake vizuri kwa hiyo kamati itamuunga mkono katika kufanya maombezi dhidi yake.
"Tumeona mwaka huu wakati anasherehekea siku yake ya kuzaliwa wananchi walimpongeza,kwahiyo nasisi anapotimiza mwaka mmoja wa Urais tutahakikisha tunampongeza kwa kufanya kongamano kubwa la kumuombea,"amesema Mtupa.
Mtupa amesema kuwa, maombi hayo yataanza baada ya wiki mbili yakianzia ofisi ya Mkuu wa Pwani kwa kumombea Mkuu wa Mkoa na baadae yataendelea katika makanisa na misikiti na hitimisho lake litakuwa kufanya Kongamano kubwa la pamoja.
Kwa upande wake Paroko wa Kanisa Katoliki la Tumbi- Kibaha, Beno Kikudo amesema pamoja na kumuombea Rais Samia lakini watafanya maombi maalum kuliombea Taifa kwa ujumla kutokana na hali ya matukio ya kiuhalifu yanayotokea nchini.
Kikudo amesema, jambo kubwa linalowasikitisha ni kuona matukio ya mauaji yakitokea katika sehemu mbalimbali ya nchi na kusema hali hiyo inawatia aibu viongozi wa dini na Taifa kwa ujumla.
"Suala la kukemea mauaji ni jukumu la watu wote na sisi kama viongozi wa dini tunalibeba na tutalikemea kwa jamii ili nchi yetu hiwe ya utulivu lakini tuwaombe wazazi wahakikishe wanawafuatilia watoto wao ili waishi katika malezi bora,"amesema Kikudo.
Kikudo amesema, kuwepo kwa ushirikiano baina ya viongozi wa dini na Serikali ambapo amemshukuru mkuu huyo wa Mkoa kwa kutoa heshima ya kukaa na kamati hiyo ili kusikiliza changamoto zao.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge katika kikao hicho amewaomba viongozi hao kuendelea kukemea vitendo vya uhalifu na kusisitiza suala la maadili kwa waumini wao.
Kunenge amesema kuwa viongozi wa dini wana mahusiano ya karibu na jamii na waumini na huwa wanasikilizwa vizuri kutokana na imani zao ndio maana Serikali inawathamini sana viongozi hao.
Amesema, Serikali ya mkoa ipo tayari kushirikiana na kamati hiyo katika kila hatua na kusema kwa sasa mkoa umepanga kutoa fursa kwao kutembelea miradi mikubwa ya kimkakati ili wajionee jinsi Serikali yao inavyofanya.
Kunenge amesema,moja ya miradi ambayo viongozi wa dini wanapaswa kutembelea ni Bwawa la Mwalimu Nyerere linalojengwa Wilayani Rufiji,Reli ya Mwendokasi,daraja la Wami pamoja na miradi mingine mikubwa inayojengwa Mkoa wa Pwani.
Mbali na hayo lakini Kunenge,amewasisitiza wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kukemea suala la mauaji,wahujumu miundombinu, kusisitiza suala la chanjo ya Uviko-19,Anuani za Makazi na Sensa.
Hata hivyo, Kunenge amesema kutokana na umuhimu mkubwa wa kamati hiyo Serikali itashirikiana nao wakati wote ikiwa pamoja na kutatua Changamoto mbalimbali zinazoikabili kamati hiyo ikiwa pamoja na kuwapatia ofisi.