Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yaridhishwa na mwenendo wa ukuaji uchumi nchini

NA GODFREY NNKO 

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema kuwa, Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imefanya kikao chake cha kawaida cha 218 tarehe 31 Januari 2022, na kupitia utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi wa ndani na wa Dunia. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BoT,Profesa Luoga amesema kuwa, kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo mzima wa uchumi, na kuidhinisha benki kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi, ili kusaidia kuendelea kuchochea ukuaji wa uchumi. 

"Msimamo huu umechukuliwa kwa kuzingatia matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3-5.

"Aidha, Kamati imeridhishwa na ukuaji wa uchumi wa Tanzania Bara, uliokua kwa wastani wa asilimia 4.9 katika robo tatu za kwanza za mwaka 2021. Ukuaji huu umechangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, kilimo, uchimbaji madini, viwanda na usafirishaji. 

"Aidha, Kamati ilibaini ongezeko la mfumuko wa bei kufikia asilimia 4.2 mwezi Desemba 2021 kutoka asilimia 3.8 mwezi Julai 2021, kutokana na changamoto za ugavi, hata hivyo mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3-5,"amefafanua Profesa Luoga.

Pia kwa mujibu wa taarifa hiyo, Profesa Luoga amesema kuwa, uchumi wa Zanzibar umekua kwa kasi ya kuridhisha kufikia asilimia 8.8 katika robo ya tatu ya mwaka 2021, ikilinganishwa na asilimia 3.3 katika kipindi kama hicho 2020, kutokana na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, hususan utalii. Mfumuko wa bei uliongezeka kidogo, ukichangiwa na bei zisizo za vyakula, hata hivyo umeendelea kubaki ndani ya lengo la chini ya asilimia 5.

"Kamati imeridhishwa na kuimarika kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kufikia asilimia 7.8 na asilimia 10 mwezi Novemba na Desemba 2021, mtawalia, kutoka chini ya asilimia 5 kwa sehemu kubwa ya mwaka 2021. 

"Mwenendo huu ni sambamba na lengo la ukuaji wa asilimia 10.6 kwa mwaka 2021/22. Ukuaji huu ulichangiwa na utekelezaji wa sera ya fedha yenye kuongeza ukwasi katika uchumi, utekelezaji wa hatua za ziada za kisera zinazolenga kuchochea utoaji wa mikopo na kushusha viwango vya riba, pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi

"Kufuatia kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Dunia. Sekta ya nje imeendelea kuimarika kutoka kwenye athari za janga la UVIKO-19, ikidhihirishwa na kurejea kwa shughuli za utalii,"amefafanua Profesa Luoga kupitia taarifa hiyo. 

Pia amebainisha kuwa, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 6.4, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa miezi sita. 

"Utekelezaji wa bajeti ya Serikali uliendana na matarajio kutokana na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato na misaada na mikopo kutoka nje. Kamati imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa ndani pamoja na wa Dunia, na hivyo matarajio ni kuwa malengo ya sera ya fedha yaliyowekwa katika Tamko la Sera ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2021/22 yatafikiwa,"amebainisha Profesa Luoga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news