NA SOPHIA FUNDI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha imepanga kutumia kiasi cha shilingi bilioni 41.8 katika mwaka wa fedha 2022/2023.Akisoma bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Mipango wa halmashauri hiyo, Rosemary Samson alifafanua kuwa kati ya kiasi hicho mishahara ni shilingi bilioni 26,095,290,000, matumizi ya kawaida sh.bilioni 2,685,519,200,miradi ya maendeleo sh.bilioni 11,927,766,800 huku mapato lindwa yakiwa sh.bilioni 1,166,424,800.
Alisema kuwa, bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 8.2 ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 ya sh.bilioni 38,264,061,000 kutokana na nyongeza ya mishahara na mapato ya ndani.
Aidha, alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya inakadiria kukusanya sh.bilioni 4.5 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Alitaja vipaumbele vya bajeti kuwa ni kumalizia miradi viporo hasa iliyotumia fedha za Serikali,kuongeza miundombinu mbalimbali katika sekta za elimu msingi na sekondari,afya na kubuni vyanzo vipya vya mapato ya ndani.
Akizungumza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Karia Magaro aliwaomba madiwani kushirikiana na wataalamu kusimamia miradi iliyotengewa bajeti katika kata zao kwani alisema jukumu la kusimamia miradi ya maendeleo katika kata ni la viongozi wa kata na vijiji wakiwemo madiwani.