NA SOPHIA FUNDI
WADAU wa Elimu wilayani Karatu mkoani Arusha wameazimia kwa pamoja kuanzisha Mfuko wa Elimu utakaowakutanisha na kutatua changamoto mbalimbali katika Sekta ya Elimu ikiwemo kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wilaya.
Wadau hao walitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha pamoja cha kujadili hali ya elimu na kutathmini matokeo ya mitihani ya upimaji na ya kitaifa kwa shule za msingi na sekondari kilichofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Karatu na kushirikisha wadau wa elimu katika wilaya hiyo.
Pia wadau waliazimia kuwepo na mafunzo ya uongozi kwa waalimu wakuu pamoja na kuwapatia walimu mafunzo ya kuwawezesha kupata maarifa ya mitaala mipya na upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi kuepuka uzururaji kwa watoto na utoro.
Akisoma taarifa ya wilaya kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji halmashauri hiyo, Afisa Elimu Sekondari, Bi.Kalista Maina amesema kuwa, hali ya ufaulu kwa wilaya imepanda kwa asilimia 88.23 kwa mwaka 2021 kwa mitihani ya Taifa kidato nne ukilinganisha na mwaka 2018/2019 ambapo wilaya ilifaulisha kwa asilimia 74.3.
Amesema kuwa, wameamua kuitisha kikao hicho cha wadau ili kupanga mikakati ya kuondoa daraja sifuri (0) kwa mitihani yote ya kidato cha nne, cha pili,darasa la Saba pamoja na darasa la nne kwa wilaya na kuongeza kiwango cha ufaulu.
Pia wilaya ilitoa zawadi mbalimbali na vyeti kwa waalimu kutoka shule za sekondari na msingi waliofanya vizuri katika masomo yao,shule zilizofanya vizuri zilizoko kwenye kumi bora kiwilaya,walimu wakuu ambao shule zao zimefanya vizuri na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao ikiwemo Shule ya Sekondari ya Ganako ambayo ilishika nafasi ya kumi bora kitaifa katika mitihani ya kidato cha sita.
Akizungumza na wadau hao, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba aliwataka wadau kuunganisha nguvu na mawazo yao kwa pamoja katika kutatua changamoto mbalimbali za elimu katika wilaya ili kuweza kuongeza kiwango cha ufaulu.
Mkuu huyo wa wilaya pia aliwataka walimu wakuu kusimamia shule zao ikiwemo kutumia muda mwingi wa kukaa shuleni kwa walimu kusimamia maendeleo ya shule na pia wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao kwani Karatu bila alama 0 inawezekana.
Mdau wa Elimu kutoka Rift Valley Children Found, Peter Mmassy alishukuru uongozi wa wilaya kwa kuwakutanisha kwani ni mwanzo mzuri wa kuitoa Karatu kuwa ya tano kimkoa kwa mitihani ya Taifa ya kidato Cha nne na kuivusha kuwa ya kwanza.
"Kwanza ni jambo la kuishukuru Serikali ya wilaya kwa kuwakutanisha kutatua changamoto za elimu kiwilaya. Kwanza wadau hatujuani kila mmoja anafanya kazi kivyake, wengine hata utakuta tunafanya kazi moja ndani ya kijiji kimoja au kata hivyo kufanya hivi leo angalau hata tumejuana na tunafanya nini na wapi,"amesema Peter.
Aliomba serikali ya wilaya kujua taasisi binafsi zilizoko ndani ya wilaya na zinafanya nini na wapi ili kuweza kuepuka taasisi zaidi ya moja kufanya kazi ndani ya kata moja kwani kuna kata zingine ambazo zina uhitaji wa miundombinu ya elimu.