NA RESPICE SWETU
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, imedhamiria kufanikisha zoezi la mfumo wa anuani za makazi linalotarajiwa kutekelezwa nchini kote.
Hali hiyo imedhihirika wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo ambacho pamoja na mambo mengine, kilikutana na kupokea taarifa na maelezo ya awali kuhusu maana na umuhimu wa mfumo huo.
Akiwasilisha taarifa ya mfumo huo kwa wajumbe wa baraza la madiwani, mwenyekiti wa kamati ya anuani za makazi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Abudius Rubatu alisema, mfumo wa anuani za makazi ni mfumo unaomtambulisha mtu mahali alipo na mahali anapofanyia shughuli zake.
Aliongeza kuwa, katika mfumo huo, barabara na njia zote zitawekewa vibao vyenye kuzitambulisha ikiwa ni pamoja na uwekaji wa namba katika kila jengo na nyumba.
Akielezea umuhimu na manufaa yatakayopatikana kutokana na mfumo huo alisema, serikali itaweza kurahisisha na kuharakisha utoaji na upelekaji wa huduma kwa wananchi.
“Manufaa megine yatakayotokana na mfumo huo ni kuwezesha kufanyika kwa biashara kwenye mitandao, kuimarisha huduma za ulinzi na usalama, kufanikisha ufanyikaji wa tafiti mbalimbali na kupunguza gharama katika huduma,” alisema.
Kufuatia kikao hicho, kamati ya mfumo wa anuani za makazi ya halmashuri ya wilaya ya Kasulu imeendelea na utoaji wa elimu kuhusu mfumo huo ambapo mpaka sasa, viongozi wa kata 21, vijiji 61 na vitongoji 283 wamefikiwa.