NA ROTARY HAULE
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chongolo amezindua barabara ya Mkombozi inayoelekea katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere na kuwataka wananchi wanaotumia barabara hiyo kuhakikisha wanaitunza miundombinu ya barabara hiyo.
Uzinduzi wa barabara hiyo umefanyika leo Februari 22, 2022 ukiwa umeshuhudiwa na makatibu wakuu wa vyama mbalimbali vya siasa kutoka nchi tano za Kusini mwa Afrika,viongozi wa CCM, wanachama na wananchi kiujumla.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita mbili inaunganisha barabara ya Morogoro katika eneo la Kibaha kwa Mfipa mpaka kufika katika Chuo cha Uongozi wa Siasa cha Mwalimu Nyerere kilichojengwa kwa ushirikiano wa pamoja na Chama Cha Kikomunisti cha Watu wa China(CPC).
Chongolo amesema, barabara ya Mkombozi imejengwa ili kurahisisha usafiri kwa wananchi na watu wengine wanaokwenda chuoni hapo na kwamba haipendezi kuona miundombinu yake inaharibiwa.
"Leo kazi yetu mimi na hawa makatibu wenzangu ni kuizindua barabara hii ili kusudi kesho viongozi wapite katika kuelekea Chuo cha Mwalimu Nyerere , lakini baada ya hapo itakuwa inatumika muda wote na wakati kwa wananchi wote,"amesema Chongolo.
Aidha, Chongolo ameeleza kusikitishwa na baadhi ya wananchi waliopo pembezoni mwa barabara hiyo kuanza kuichafua kwa kutupa taka katika mtaro wa barabara hiyo huku akisema jambo hilo halitavumilika.
"Jana tulikuwa tunapita katika barabara hii lakini tuliona watu wametupa taka katika mtaro jambo ambalo si sawa, lakini nawaomba tujitahidi kutunza miundombinu ili kuepusha uharibifu na kuifanya barabara hiwe safi na kupitika wakati wote,"amesema Chongolo.
Aidha, kuhusu chuo cha Mwalimu Nyerere Chongolo amesema kuwa ujenzi wa chuo hicho ni fursa kwa wananchi wa Tanzania,na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika katika kuwanoa viongozi na hata kuwaandaa viongozi wa baadae.
Chongolo,amewataka viongozi wa Mkoa Pwani kuhakikisha wanaandaa programu maalum ambayo itawasaidia wananchi wanaokizunguka chuo hicho kupata fursa ya kushiriki mambo mbalimbali yanayotolewa chuoni hapo.
"Leo tumezindua barabara hii lakini kesho Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anakuja kuzindua Chuo cha Mwalimu Nyerere kwahiyo niwaombe sana wanaPwani na wananchi wa hapa Kibaha kuona umuhimu wa kukitumia chuo hiki kama fursa ya kujiletea maendeleo,"ameongeza Chongolo.
Kwa upande wake mbunge mstaafu wa Viti maalum mkoa wa Pwani, Zainabu Vullu,amepongeza juhudi za Serikali na chama kupitia Rais Samia kwa kukamilisha ujenzi wa chuo hicho.
Vullu amesema kuwa, chuo hicho kitasaidia kuimarisha viongozi kwa kuwajengea uweledi,uadilifu,uaminifu wa kutumikia nafasi zao na hata katika kuwaandaa viongozi wengine wa baadae.