NA ROTARY HAULE
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo kesho Februari 22 anatarajia kuwaongoza Makatibu Wakuu wenzake watano wa vyama vya siasa kutoka nchi za Kusini mwa Afrika katika ufunguzi wa barabara ya Mkombozi (Mkombozi Road) iliyopo Kibaha kwa Mfipa inayoelekea katika chuo cha uongozi wa Siasa Cha Mwalimu Julius Nyerere.
Makatibu hao wanatoka katika vyama mbalimbali kikiwemo Chama Cha MPLA ( Angola),ANC (Afrika Kusini),ZANUPF ( Zimbambwe),SWAPO (Namibia), FRELIMO ( Msumbiji) pamoja na wenyeji (CCM).
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Pwani, Said Goha ametoa taarifa hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo chuoni hapo na kwamba ufunguzi wa barabara hiyo ya Kilomita 2 ni sehemu ya maandalizi ya ufunguzi wa chuo hicho utakaofanywa na Rais Samia Februari 23.
Goha amesema kuwa, Chongolo ataambatana na viongozi hao kwa kuwa vyama vyao ni miongoni mwa vyama vilivyoshiriki harakati za masuala ya ukombozi wa kupigania Uhuru katika nchi za Kusini mwa Afrika na kusema barabara hiyo imejengwa na Chama Cha Kikomunist cha watu wa China(CPC).
Amesema kuwa,baada ya uzinduzi wa barabara hiyo kukamilika itafuatia na sherehe kubwa ya uzinduzi wa chuo hicho utakaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan Februari 23 .
Amesema,hali ya maandalizi ya shughuli zote yanakwenda vizuri ikiwa pamoja na upande wa uzinduzi wa barabara na hata uzinduzi wa chuo hicho na kusema usimamizi wa karibu unaendelea kwa ajili ya kuweka sawa mambo madogo madogo.
"Siku ya kesho tutakuwa na shughuli ya uzinduzi wa barabara ya Mkombozi Road utakaofanywa na Katibu Mkuu comred Daniel Chongolo kwa kushirikiana na makatibu wenzake wa nchi tano Februari 23 tutakuwa na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kufungua chuo cha Mwalimu Nyerere ,kwahiyo niseme tu maandalizi yote yanakwenda vizuri,"amesema Goha.
Goha amesema, chuo hicho ni chuo cha uongozi na kitatoa elimu ya uongozi kwa wanachama wa CCM na wasiokuwa wanaCCM na kusema lengo kubwa la kuanzisha chuo hicho ni kuwajengea uwezo wananchi wote.
"CCM imeanzisha chuo hiki kwa ajili ya kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania na walio nje ya Tanzania ili waongeze weledi,kwa maana ya nidhamu,maadili,uadilifu na uzalendo kwa nchi zao,"amesema Goha.
Goha amewaomba wanachama wa CCM pamoja na wakazi wa Mkoa wa Pwani kiujumla kujitokeza kwa wingi katika kumlaki Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wageni wengine watakaokuja Pwani kwa ajili ya uzinduzi wa chuo hicho.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amepongeza juhudi na kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia na kusema uwepo wa chuo hicho kutasaidia kufungua fursa za uchumi kwa wananchi wa Kibaha , Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Kunenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama alisema mkoa unatambua kuwepo kwa ugeni mkubwa na kwamba hali ya Ulinzi na Usalama ipo vizuri itazidi kuimarishwa siku hadi siku ili kusudi mambo yaende kadri yalivyopangwa.
"Mkoa wetu unapokea ugeni mkubwa na kuanzia Februari 22 tutakuwa na Makatibu wakuu wa vyama vya Siasa kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika na Februari 23 tutakuwa na ugeni mkubwa wa Rais Samia katika uzinduzi wa chuo kwahiyo Mkoa wetu upo salama na hakuna shaka juu ya wageni wetu,"amesema Kunenge.
Kunenge amesisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika shughuli hizo kwa ajili ya kumlaki Rais Samia na kwakuwa ni kiongozi mahiri na shupavu ambaye mwenye kufanyakazi ya kuwaletea maendeleo Watanzania.