KMC FC: Tuna jambo letu dhidi ya Dodoma Jiji FC pale Chamanzi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MCHEZO wa KMC FC wa Ligi kuu ya NBC Soka Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji uliopangwa kuchezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili ya Februari 20,2022 umehamishwa na sasa utapigwa katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamanzi jijini Dar es Salaam saa moja kamili jioni.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Februari 18, 2022 na Afisa Habari na Mawasiliano wa KMC FC, Christina Mwagala.

"Kwa mujibu wa barua ya Bodi ya Ligi (TPLB) iliyotumwa jana mchana, ili ieleza klabu kuwa mabadiliko hayo yanatokana na Uwanja wa Benjamin Mkapa kuwa na matumizi mengine siku hiyo ya Jumapili ya Fabruari 20 na hivyo kuhamishiwa Azam Complex.

"Kama klabu tumepokea kwa mikono miwili mabadiliko hayo na tunawaomba mashabiki na Watanzania wote waliojiandaa kwenda kuwasapoti wachezaji kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa wajitokeze kwenye uwanja wa Azam Complex kama ambayo barua ya TPLB ilivyoelekeza mabadiliko ya mchezo huo,"amefafanua Bi.Mwagala.

Pia amesema, kwa upande wa maandalizi ya mchezo huo yameendelea kufanyika kwa umahiri mkubwa na kwamba wachezaji pamoja na benchi la ufundi wamejiandaa kufanikisha timu kupata ushindi na hivyo kuondoka na alama tatu muhimu kwani mchezo huo upo ndani ya uwezo wao.

"Aidha katika kipindi ambacho timu zilikuwa mapumziko ya kupisha michuano ya Kombe la Azam Sport Federation, KMC FC haikuvunja kambi na hivyo wachezaji wote waliendelea kukaa kambini sambamba na kufanya mazoezi kutokana na mpango maalumu ambao Kocha Mkuu Thierry Hitimana alikuwa ameuandaa.

"Miongoni mwa mipango ya maandalizi ya Kocha Mkuu Hitimana ilikuwa ni kufanya mazoezi sambamba na kucheza mechi za kirafiki na mchezo wa kwanza ulikuwa ni dhidi ya Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC Soka Tanzania Bara ambapo KMC ilipata ushindi wa magoli matatu kwa sifuri,"amesema.

Bi.Mwagala amefafanua kuwa, timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni ilicheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya JKT Tanzania ambayo inashiriki Ligi ya Championship ambapo KMC ilipata ushindi wa magoli sita kwa sifuri.

Amesema, michezo hiyo ililenga kuwajenga wachezaji sambamba na kurekebisha makosa mbalimbali yaliyojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Biashara United ya Musoma mkoani Mara uliomalizika kwa sare ya goli moja kwa moja, lakini pia kujiweka vizuri kwenye mchezo muhimu dhidi ya Dodoma Jiji.

“Katika kipindi hiki ambacho tulikuwa kwenye mapumziko, tumekuwa na muda mzuri wa kufanya maandalizi, na sasa tupo kwenye hatua ya mwisho kabla ya mchezo wetu wa Jumapili, kikubwa mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Azam Complex ili kuwapa sapoti wachezaji wetu, tunawaahidi kufanya vizuri na kupata ushindi,"ameongeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news