Kuelekea mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani: Maliasili na Utalii yaanika mafanikio

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt.Damas Ndumbaro amesema kuwa,tangu Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aingie madarakani Sekta ya Maliasili na Utalii imeendelea kukuwa kwa kasi na kuna mafanikio mengi wanajivunia.

Dkt.Ndumbaro ameyasema hayo leo Februari 26, 2022 kupitia mjadala wa Kitaifa ulioratibiwa na Watch Tanzania kwa udhamini wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) huku mada ikiwa ni Maendeleo katika Sekta ya Utalii kuelekea mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani.

Mjadala huo ambao umewakutanisha pamoja viongozi na wadau mbalimbali wa Sekta ya Maliasili na Utalii kutoka ndani na nje ya Tanzania kupitia Mtandao wa Zoom umerushwa mubashara kupitia runinga mitandao.

Mheshimiwa Waziri Dkt. Ndumbaro amesema kuwa, Sekta ya Maliasili na Utalii ni muhimu sana katika uchumi wa nchi, kwani kabla ya UVIKO-19 ilikuwa inachangia asilimia 21 ukichanganya maliasili na utalii.

"Lakini, tangu Mheshimiwa Rais Samia, Rais wa Awamu ya Sita aingie madarakani, tumepata mafanikio mengi katika sekta hii, tunafahamu wakati anaingia alikuta kipindi kigumu sana katika sekta ya utalii kwa. Kwa sababu tulikuwa tunasumbuliwa na ugonjwa wa UVIKO-19.

"Lakini, pamoja na hayo tumepata mafanikio mengi sana, kwanza tumeweza kutambulika na jumuiya ya Kimataifa, yaani Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Utalii (UNWTO). Kwamba Tanzania ni nchi ambayo imefanya vizuri zaidi katika kipindi cha UVIKO-19. Yaani the most resilient country during Covid-19 (nchi yenye ustahimilivu zaidi wakati wa UVIKO-19). Kwa hiyo ni heshima ambayo tumepewa na taasisi ya Umoja wa Mataifa.

"Na tulipewa tukiwa kule Spain, lakini pia idadi ya watalii tangu Mheshimiwa Rais Samia aingie madarakani imeongezeka, takwimu za 2020 zinasema wazi kuwa,  tulikuwa na watalii laki sita na ishirini (620,000), lakini takwimu za 2021 tuna watalii wa nje laki tisa na ishirini na mbili (922,000) na watalii wa ndani laki saba na themanini na nane (788,000).

"Na jumla kwa mwaka huo kipindi cha UVIKO tumepata watalii milioni moja pointi saba (1,700,000). Kwa  watalii wa ndani pamoja na kipindi cha UVIKO, tumeweza kuvunja rekodi ya idadi ya watalii wa ndani tangu tupate Uhuru, yaani huko nyuma hakuna UVIKO-19, lakini hatukuweza kufikia idadi hii ambayo tumefikia kipindi hiki, kwa hiyo tumefanya vizuri tangu Mheshimiwa Samia aingie madarakani.

"Na ukiangalia ongezeko,kwa mwaka 2020/21 ni ongezeko la asimia 40.2 kwa hiyo tumefanya vizuri tangu mheshimiwa Rais Samia ameingia madarakani kwa ongezeko la asilimia 40.2,"amefafanua Dkt.Ndumbaro.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Ndumbaro amesema, pia kwa upande wa mapato yatokanayo na Sekta ya Maliasili na Utalii yameongezeka kwa kasi.

"Kwa mwaka 2020 mapato yatokanayo na watalii wa ndani yalikuwa ni bilioni tisa (shilingi bilioni 9), lakini 2021 mapato ya watalii wa ndani ni bilioni 12.4 (shilingi bilioni 12.4).

"Lakini hata mapato ya watalii kutoka nje mwaka jana (2020) yalikuwa ni dola za Marekani milioni 745 lakini 2021 tumepata dola za Kimarekani bilioni 1.24. Unaona haya ni mafanikio ya kitakwimu ambayo mtu yoyote hawezi kwenda na kuyabeza,ambayo yanaonekana kuna ongezeko na ufanisi chanya katika Sekta ya Utalii,"amefafanua Mheshimiwa Dkt.Ndumbaro.

Pia amesema,mafanikio mengine ni pamoja na Tanzania kupewa heshima ya kuwa mwenyeji wa kwanza katika Onesho la Utalii katika nchi za Afrika Mashariki.

"Niseme wazi kuwa, hii heshima tulipata kwa sababu ya heshima ya Rais Samia, kwa sababu katika hali ya kawaida tulipaswa kwenda katika 'Alphabetical order' na T si ya kwanza katika mtiririko huo.Lakini, kwa kutambua mchango wa Mheshimiwa Rais Samia katika sekta hii, tukapewa nafasi hiyo,"amesema.

Mheshimiwa Waziri ametaja mafanikio mengine kuwa,kwa mwaka 2021 wamepata tuzo 14 kutoka katika taasisi mbalimbali za Kimataifa. "Tuzo hizo ni ndani ya mwaka mmoja ikiwa ni heshima kubwa sana,"amesema.

Wakati huo huo, Dkt.Ndumbaro amesema kuwa, juhudi za Rais Samia katika kuhakikisha Sekta ya Utalii inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa zimeanza kuzaa matunda, kwani kupitia filamu ya Royal Tour ambayo aliiandaa hivi karibuni ingawa bado haijazinduliwa mambo mazuri yameanza kuonekana.

Amesema, tayari kampuni 30 za mawakala wa utalii kutoka Marekani na Ulaya zimekuja nchini baada ya kuona vipande vya filamu hiyo inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

"Pia tumezindua utalii wa michezo mfano timu ya Yanga ilivaa jezi zimeandikwa Visit Kilimanjaro na Zanzibar ila pia timu ya Simba ambayo ipo kwenye mashindano makubwa Afrika inavaa Visit Tanzania hii ni hatua kubwa sana,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Ndumbaro.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Dkt.Ndumbaro amesema kuwa, bajeti yao ya mwaka 2021/2022 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametekeleza kwa mafanikio kwa maana ya asilimia 80 ikiwa bado asilimia 20 ambazo zipo katika utekelezaji kwa sasa.

NCCA

Naye Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dkt.Freddy Manongi amesema, mikakati ya Rais Samia katika kuistawisha Sekta ya Maliasili na Utalii imewezesha mamlaka hiyo kusonga mbele ikizingatiwa kuwa, UVIKO-19 ulizorotesha mapato.

Amesema, UVIKO-19 uliweza kuathiri mapato kwani pato liliporomoka kutoka shilingi bilioni 102 hadi bilioni 31.

"Ila tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alitupa shilingi bilioni 6.6 katika kupambana na athari za UVIKO-19 na hasa katika miundombinu,"amesema.

Amebainisha kuwa, hifadhi hiyo ina tatizo kubwa la mwingiliano wa watu na wanyama, hivyo kupitia fedha hizo ambazo Rais Samia aliwapatia wanajitahidi kutengeneza miundombinu mbalimbali ambayo itaongeza pato katika hifadhi.

Dkt.Manongi ameongeza kuwa, wakati Mheshimiwa Rais Samia akirekodi filamu ya Royal Tour alifika katika Hifadhi ya Ngorongoro kuwatembelea.

"Na tulifarijika sana,kupitia Royal Tour tumeweza kupata wawekezaji kadhaa kwa ajili ya kuja kuwekeza katika hifadhi yetu (Hifadhi ya Ngorongoro),"amesema Dkt.Manongi.

Bodi ya Utalii

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bw. Felix John Michael amesema kuwa, kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia, bodi hiyo ina mafanikio mengi ya kujivunia.

Amesema kuwa, miongoni mwa mafanikio waliyoyapata ni pamoja na kushiriki maonesho mengi ya ndani ambayo ni sehemu ya mikakati yao ya kuhakikisha wanavitangaza zaidi vivutio vya utalii.

Miongoni mwa maonesho hayo amesema ni Senene Festival,Sabasaba, Majimaji Serebuka, Burigi huko Chato, Bagamoyo Cultural Festival na mengineyo.

Amesema, ushiriki wao katika maonesho ya ndani na nje ya nchi unalenga kutoa elimu ikiwemo kuhamasisha utalii wa ndani na nje juu ya vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo hapa nchini.

"Tumekuja na mbinu ya kupanda mbegu ya kupenda na kudhamini vivutio vyetu vya utalii, hivyo tutatembelea vyuo mbalimbali pamoja na kambi za jeshi kwa wale wanaofanya mafunzo ya jeshi ili kuelimisha na kufundisha faida za vivutio vyetu,"amesema Bw.Michael.

TANAPA

Kamishna wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), William Mwakilema anasema kuwa, kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia kuna mambo mengi ya kujivunia.

Jambo la kipekee zaidi, Kamishana Mwakilema anasema ni kuimarika kwa uhifadhi kupitia ulinzi wa rasilimali za Taifa.

"Na kupitia kile kipindi cha Royal Tour ambacho yeye ndiye tour guide namba moja wa kuelekeza Watanzania na Dunia nzima kwamba Tanzania tunafanya vizuri. Hii imeleta mafanikio makubwa mno katika Sekta ya Utalii nchini.

"Utalii unapofanyia maeneo mbalimbali ya nchi, kuna uwekezaji ndani ya hifadhi za Taifa ambazo hao wadau pia wameajiri watu wengi kwenye hoteli. Makambi (kambi) ya watalii na usafirishaji.

"Pamoja na ajira binafsi, kuna mama ntilie wanauza chakula, hizo ni ajira ambazo zimetokana na watalii. Pia kutokana na shughuli za utalii kuendana na ajira, kama TANAPA tumeweza kutoa ajita takribani kwa watumishi 2983 na hizo ni ajira za moja kwa moja,"amefafanua Kamishna Mwakilema.

Ameongeza kuwa, juhudi za Mheshimiwa Rais Samia zilizofanikisha kupata fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za UVIKO-19 katika sekta mbalimbali nchini zimewezesha na wao TANAPA kupata  shilingi Bilioni 46.792 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu mbalimbali ya hifadhi.

UNESCO

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), Profesa Hamis Malebo amesema kuwa, kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia kuna mafanikio mengi ikiwemo Tume ya Tafa ya UNESCO kwa kushirikiana na mwakilishi wa kudumu wa UNESCO Tanzania imefanikiwa kukipitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya UNESCO na Umoja wa Mataifa.

Amesema, uamuzi huo utasaidia zaidi katika sekta ya utalii huku akiainisha kuwa, pia Tanzania imeingiza maeneo saba katika urithi wa Dunia.

Profesa Malebo ameyataja maeneo hayo kuwa ni Songo Mnara,Ngorongoro,Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani, Pori la Akiba la Selous,Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, eneo la michoro la Miambani Kondoa na Mji Mkongwe Zanzibar.

Aidha, amesema tume hiyo ilitafuta fedha zaidi ya milioni 50 kwa ajili ya maeneo ya urithi wa Dunia ambayo yalikuwa hayaendi vizuri kiuhufadhi na yaliyokuwa na changamoto kadhaa ikiwemo magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ambayo yalikuwa yanaharibiwa na mawimbi ya maji.

"Pia maeneo ambayo yamekuwa na changamoto za uhifadhi mojawapo ni Serengeti, kumekuwa na ushoroba ambao kwa miaka mingi umevamia na wananchi na wakulima, lakini ni njia ya muhimu sana ya wanyama kwenda katika eneo Victoria kunywa maji na hilo limeleta changamoto za uhifadhi na tume imeshatoa ushauri wa namna ya kuokoa hili,"amesema Profesa Malebo.

Aidha, amesema kuwa, Tume ya UNESCO imebaini kuwepo kwa changamoto za kiusalama katika Hifadhi ya Ngorongoro kwani watoto hawawezi kwenda shule salama.

"Siku zote kuna changamoto za kumakwatwa na chui,simba na fisi pamoja na akinamama ambao wanakwenda kusanya kuni wamekuwa wakikumbana na wanyamapori na akina baba, kwa hiyo usalama si mzuri na tume tumeshauri kwa Serikali waweze kuwatafutia maeneo mengine ili waweze kuondokana na hizo changamoto,"amesema Profesa Malebo.
TAZAMA WACHANGIAJI WAPYA NA MIJADALA ZAIDI HAPA CHINI

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news