Kwa nini Wabunge hawajapoteza kura kwa Dkt.Tulia Ackson?

NA GODFREY NNKO

NI kwa sababu wametambua ni mtu sahihi katika wakati sahihi wa kuuongoza mhimili huo muhimu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pengine tunaweza kusema leo, Februari 1, 2022 Dokta Tulia Ackson ameandika historia nyingine katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa Spika wa pili mwanamke na Spika wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alitanguliwa na Chief Adam Sapi Mkwawa mwaka 1962 hadi 1973, Chief Erasto Mwang'enya mwaka 1973-1975, Chief Adam Sapi Mkwawa mwaka 1975 hadi 1994, Pius Msekwa mwaka 1994-2005,Samuel John Sitta kati ya mwaka 2005 hadi 2010, Anne Semamba Makinda-2010 hadi 2015, Job Yustino Ndugai 2015 hadi 2021ambapo alijiuzulu nafasi hiyo.

Akiwa kiongozi asiyekuwa na makuu, anayejali makundi yote katika jamii, Dkt.Tulia ambaye kitaaluma ni Mwanasheria mara ya kwanza kuanza kujulikana nje ya duru za kisheria ilikuwa ni Februari mwaka 2014, wakati Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alipomteua kuingia katika Bunge Maalumu la Katiba akiwakilisha Jumuiya na Taasisi za Elimu ya Juu. 

Aidha, ni Dkt. Jakaya Kikwete ndiye pia aliyemteua Mheshimiwa Dkt.Tulia kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilipofika Septemba mwaka 2015.

Kwa taaluma yake, nafasi hiyo inatajwa kumfaa zaidi kwa sababu Baraza la Kutunga Sheria au Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina sehemu mbili, yaani Rais na Wabunge. 

Rais anatekeleza madaraka yote aliyokabidhiwa na Katiba kwa kuridhia miswada ya sheria ya bunge ili kukamilisha mchakato wa kutunga sheria kabla ya kuwa sheria, hivyo anapopatikana mbobezi wa masuala ya kisheria mambo ya Bunge yanakwenda kwa kasi na ufanisi mzuri.

Dkt.Tulia amepewa dhamana ya kuliongoza Bunge ambalo ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kina madaraka kwa niaba ya wananchi, kusimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake. 

Bunge lina aina nne za wabunge, kwa maana ya wabunge waliochaguliwa moja kwa moja kuwakilisha majimbo ya uchaguzi Tanzania Bara na Zanzibar; wabunge watano waliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi kutoka miongoni mwa wajumbe, Mwanasheria Mkuu; wabunge wasiozidi 10 walioteuliwa na Rais na wabunge wanawake wasiopungua asilimia 15 ya makundi mengine yote kwa msingi wa uwiano wa uwakilishi miongoni mwa vyama vilivyopo katika Bunge.

Dkt.Tulia anakuwa Spika baada ya kukaimu nafasi ya Uspika kwa zaidi ya miezi sita ambayo aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai alikuwa akikabiliwa na changamoto za kiafya baada ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Dkt.Tulia Ackson ambaye alikuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo aliiongoza nafasi hiyo kwa ufanisi na weledi mkubwa ingawa alikuwa ni spika asiye na cheo cha kuthibitishwa.

Ufanisi huo, ulionekana wa kipekee zaidi kwa kutekeleza majukumu ambayo Spika wa Bunge hawezi kumwaachia Naibu Spika wake ayatekeleze.

Leo Mheshimiwa Dkt.Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ufanisi wake umethibitishwa baada ya kuaminiwa kwa asilimia 100 na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumpa kura zote.

Ni kupitia uchaguzi uliofanyika leo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao uliongozwa na mwenyekiti ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa, Mheshimiwa William Lukuvi.

Akitangaza matokeo baada ya wagombea kujieleza na kura kupigwa,Mheshimiwa William Lukuvi amesema,Dkt.Tulia amepata kura 376 kati ya kura 376 zilizopigwa na wabunge ambapo wagombea wenzake nane wameambulia sufuri.

“Dkt. Tulia Ackson huyu ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amepata kura zote 376,” amesema Mheshimiwa Lukuvi huku wabunge wakishangilia.

Mheshimiwa Lukuvi amesema, wapiga kura walikuwa wabunge 376 na hakuna kura iliyoharibika huku wagombea wengine wote nane wakiwa hawajapata kura yoyote.

Wagombea wengine waliokuwa wakichuana na Dk Tulia ambaye alikuwa Naibu Spika wa Bunge ni pamoja na Abdullah Mohamed Said (NRA), Aivan Maganza (TLP), Daivd Mwaijojele (CCK) na Georges Busungu (ADA-TADEA), Kunje Ngombale Mwiru (SAU), Maimuma Said Kassim (ADC), Ndonge Said Ndonge (AAFP) na Saidoun Abrahamu Khatibu.

Aidha, baada ya kuchaguliwa, Dkt.Tulia alikula kiapo na baadaye kutoka nje ya ukumbi kuvaa vazi la Spika na kurejea ndani kuendesha kikao cha Bunge.

Kabla ya kuanza kuendesha kikao chake cha kwanza akiwa Spika, Dkt.Tulia alianza kumuapisha Mbunge mpya wa Ngorongoro, Emmanuel Shanghai.

Shanghai alichaguliwa baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, William Ole Nasha ambaye alifariki mwaka jana akiwa nyumbani kwake jijini Dodoma.

Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi amesema uchaguzi huo umefanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri nya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 84.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news