Maafisa biashara watakiwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara

NA CHRISTINA NJOVU-BRELA

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.Mhandisi Robert Gabriel amewataka Maafisa Biashara nchini kutoa elimu kwa wafanyabiashara kwa kufungua dirisha la biashara la ukuaji sekta ya biashara ili kufufua matumaini kwa wafanyabiashara na kurudi katika biashara zao. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi, Robert Gabriel, akifafanua jambo wakati akifungua mafunzo ya Maafisa Biashara wa mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na Simiyu. Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoandaliwa na BRELA yameanza Februari 7, 2022 jijini Mwanza na yatahitimishwa Februari 11, 2022.(Picha na BRELA).

Mhandisi Gabriel ametoa wito huo Februari 7, 2022 wakati wa kufungua mafunzo juu ya Sheria za Leseni za Biashara kwa Maafisa Biashara wa mikoa ya Kanda ya ziwa ikiwemo mikoa ya Kagera, Geita Mwanza, Mara na Simiyu yanayoendeshwa na Wakala ya Usajili biashara na Leseni (BRELA) kwa muda wa siku tano mkoani Mwanza.

Mhe. Gabriel amesisitiza umuhimu wa Maafisa Biashara kutoa elimu kwa wananchi ambayo ni nyenzo muhimu ya kupunguza kero mbalimbali na gharama za urasimishaji biashara, suala mbalo Serikali imekuwa ikilipigia kelele kwa nguvu zote.

“Ndugu zangu Maafisa Biashara kuna mtu amepata mtaji anataka aanze biashara mapema lakini unamuambia njoo kesho mara kesho kutwa anachanganyikiwa, tukumbuke kuwa mteja ni mfalme,” amefafanua Mhe. Gabriel.
Baadhi ya Maafisa Biashara wa mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na Simiyu. wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya Sheria ya Leseni za Biashara. Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) yalianza Februari 7, 2022 jijini Mwanza na yatahitimishwa Februari 11, 2022.(Picha na BRELA).

Aidha aliongeza kuwa ikiwa mfanyabiashara huyo ataambiwa njoo kesho mara kesho kutwa, utakuta fedha aliyonayo inapata matumizi mengine na kuiingiza katika kutatua changamoto aliyonayo kiasi kwamba anakwama katika kutimiza malego yake, Afisa biashara unapoonekana mahali uonekane kuwa ni msaada kwa wafanyabiashara, hivyo watatulieni changamoto zao. 

“Fungueni dirisha maalum la kutatua changamoto za wafanya biashara na mnatakiwa kujipima kwa kila robo ya mwaka, msifanye kazi kwa mazoea (business as usual ), kuweni na takwimu kuwa nina wafanya biashara wadogo wangapi, wakubwa wangapi na wale walio ICU ni wangapi na kutafuta njia ya kuwasaidia ili waweze kurudi katika hali zao za kibiashara,” amesisitiza Mhandisi Gabriel.

Ameongeza kuwa kwa utafiti mdogo uliofanyika kuhusu utendaji kazi wa Maafisa Biashara umebaini kuwa kumekuwa na uelewa hafifu wa Sheria ya Leseni za Biashara sura ya 208, na Maafisa Biashara wengi kutumika kama wakusanyaji mapato hasa vilabuni, maduka makubwa na nyumba za kulala wageni, kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kazi wazifanyazo haziusiani na majukumu yao. 

Mhe. Gabriel amesema ni vema Maafisa Biashara wakafuatilia mafunzo hayo ambayo hayajaandaliwa kwa bahati mbaya bali ni mkakati maalumu wa kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na Maafisa Biashara zinatoa nafasi kwa wafanyabiashara kuimarika kibiashara na kupata fursa ya kushiriki katika kuchangia pato la taifa ambalo litatumika kutoa huduma kwa wananchi katika mkakati mahususi wa blue print. 

Amewataka Maafisa biashara kuleta faida ya mafunzo haya kwa kuandaa mpango kazi maalumu , Mafunzo haya ya siku tano yatoe matunda, mafunzo haya yakawe kimpango kazi na kuonesha muelekeo mzima wa utatuzi wa changamoto na ongezeko la wafanya biashara na kukuza biashara nchini. 
" Leseni za Biashara kundi "A" zinatakiwa kutolewa na BRELA na si Maafisa Biashara, Wanaofanya hivyo wanakiuka utaratibu na kusababisha Serikali kupoteza mapato"
Godfrey Nyaisa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA. (Picha na BRELA).

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kufungua mafunzo hayo amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo kwa wafanya biashara ni kuwajengea uwezo maafisa biashara wa mikoa na halmashauri zote nchini ili waweze kuielewa vema Sheria ya Leseni za Biashara sura namba 208 na kuweza kutoa huduma bora kwa wafanyabiashata na kusaidia kutoa huduma za Serikali kwa wananchi hatimaye kuboresha mazingira ya biashara nchini. 

Hata hivyo Bw. Nyaisa amekemea baadhi ya Maafisa Biashara ambao wanatoa leseni kundi “A” ambazo zinapaswa kutolewa na (BRELA), kwa kuwaeleza kuwa; Katika kaguzi za Leseni za Biashara zinazofanywa na BRELA katika maeneo mbalimbali nchini, imebainika kuwepo kwa baadhi ya maafisa hao katika Halmashauri ambao wamekuwa wakitoa leseni za biashara kundi “A” zinazotakiwa kutolewa na BRELA kwa mujibu wa sheria ya Leseni za Biashara na kwa kufanya hivyo huu ni uvunjifu wa sheria na pia inasababisha Serikali kupoteza mapato yake na kuwataka kuacha mara moja na ikiwa hali hiyo itaendelea taarifa zitatolewa kwa mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. 

Bw. Nyaisa ameongeza kuwa BRELA inaendelea na uboreshaji wa utoaji wa huduma zake na kuweka mazingira wezeshi ya biashara nchini, kwa sasa huduma zote za BRELA zinapatikana kwa njia ya mtandao kupitia mifumo miwili unaojulijana kama ONLINE Registraton System (ORS) kwa Sajili na Leseni za Viwanda na Tanzania National Business Portal (TNBP) kwa utoaji wa Leseni za Biashara. Aidha mfumo wa utoaji wa Leseni za Biashara (National Business Portal-NBP) unafanyiwa maboresho ili uweze kutumika kutoa huduma za Leseni za Biashara katika Halmashauri zote nchini kwa utoaji wa Leseni za Bishara kundi “B” ambapo hatua hii itaboresha mazingira ya biashara nchini na kuwapunguzia gharama wajasiriamali na wafanyabiashara. 

Aidha, amewataka Maafisa Biashara kubadilika kama ambavyo wito umekuwa uitolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuwasisitiza watumishi wa umma kubadilika na kuwa mfano bora kwenye utendaji kazi na uwajibikaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news