NA FRESHA KINASA
MACHIFU wa Mkoa wa Mara wameiomba Serikali iweze kuwatambua na kuwathamini ili washirikiane kwa pamoja kusaidiana katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kusimamia suala la amani, usalama na kukomesha vitendo vya mauaji ambavyo hivi sasa vimeonekana kushamiri nchini.
Wameyasema hayo leo Februari 3, 2022 wakati wakizungumza na waandishi wa habari Mjini Musoma ambapo pamoja na mambo mengine, wamesema kuwa iwapo Serikali itashirikiana nao kwa karibu kutasaidia kuimarisha amani, usalama na maadili mema kwa jamii na vitendo vya kihalifu pamoja na kukomesha mauaji ambayo kwa sasa yanaonekana kushamiri.
Japheti Wanzagi ni Chief kutoka kabila la Wazanaki amesema kuwa, machifu ni wapatanishi na walinzi wa amani ikiwemo kupatanisha na kuangalia mienendo inayofaa ndani ya jamii hivyo Serikali ishirikiane nao kwa karibu kwa kuwashirikisha katika mikutano mbalimbali muhimu ihusuyo masuala ya kijamii, utatuzi wa migogoro, kwa maslahi mapana ya nchi.
"Hata kabla ya Uhuru enzi na enzi machifu walitumika kusuluhisha migogoro mbalimbali na kusimamia maadili katika jamii zao. Walionya, kukemea maovu na kudhibiti tafrani, kwa hiyo machifu wathaminiwe kama ilivyokuwa nyuma, Serikali ione umuhimu wa machifu katika jamii, leo hii mauaji yanatokea, lakini kuna haja ya Serikali kuwaita na kuwashirikisha kumaliza vitendo hivyo,'" amesema Chifu Wanzagi.
Kwa upande wake Chifu Deus Masanja kutoka Bunda Himaya ya Sizati amesema kuwa, Machifu wana mchango wa kudumisha amani hata awali walisaidia jamii maadili mazuri, walikuwa msaada kusaidia tawala zilizopo madarakani na pia ameomba Serikali kutowasahau hata kidogo kwani wana uwezo wa kusaidia kuondoa mikosi na laana ambazo zinatokea katika jamii.
Ameongeza kuwa, Machifu mkoani Mara wataendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu kwa moyo wa upendo kabisa na katika uongozi wake kusudi azidi kufanikisha ajenda ya kuleta maendeleo katika taifa.Huku pia wakiomba Watanzania wote kumpa ushirikiano wa dhati Mheshimiwa Rais Samia.
"Tunamkaribisha Rais Samia tarehe 5/2/2022 huyu ni chifu mwenzetu Hangaya tutashirikiana naye na kumtetea kwa aina yoyote mchana na usiku wapo watu wanazusha kuwa eti uchifu ni uchawi huo ni upotoshaji mkubwa kabisa, kwani nyuma walikuwepo machifu Isike, Mirambo, Odemba, Makongoro ambao walifanya kazi kubwa na nzuri katika maeneo yao na kuleta heshima kubwa tu,"amesema Chifu Masanja.
"Tunakemea mauaji ya watu yanayotokea sehemu mbalimbali nchini, kwani hayafai hata kidogo na tushirikiane sote kuyatokomeza. Wapo baadhi ya Wakuu wa Wilaya hawatutambui kama tunafaida katika jamii, tunaomba tushirikiane nao, wapo wanadai uchifu ulifutwa zana hii haina ukweli wowote. Vijana wanaoletwa kama viongozi ndio wanaona kama tunawaingilia pindi tunapowapa ushauri,"amesema.
Naye Chifu Msangya Ongati wa Rorya Himaya ya Kiseru amewaomba makamanda wa Polisi wa mikoa mbalimbali yanapotokea mauaji katika maeneo yao wawaite Machifu na Wazee wa Kimila kupata ufumbuzi kwani baadhi ya mauaji yanatokea kutokana na watu wanaofanya vitendo hivyo kuwa na laana kutoka kwenye koo zao, hivyo wazee wa Kimila wana mwarobaini juu ya matatizo iwapo wakishirikishwa.
"Yanapotokea mauaji, kamanda wa Polisi wakae meza moja na Machifu na Wazee wa kimila kujua zaidi kwa nini mauaji yanatokea, yawezakuwa kuna upepo mbaya unaweza kuingia kwenye Serikali, nchi au eneo husika ukaleta mambo mabaya, lakini Machiefu wakiitwa watasaidia sana kwani wamewekwa na Mungu katika Jamii na Wala sio wachawi kama baadhi wa watu wanavyodhani,"amesema.