*Aagiza tathmini ifanyike kuhusu matumizi ya cable car mlima Kilimanjaro
NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha sekta ya michezo nchini inapiga hatua kwenda mbele kwani michezo ni zaidi ya burudani.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizngumza wakati alipofunga maadhimisho ya Kilimanjaro Marathon kwenye uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi, Februari 27, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Ametoa kauli hiyo leo
Februari 27, 2022 alipozungumza na wananchi wakati wa maadhimisho ya
miaka 20 ya Kilimanjaro Marathon 2022 katika Uwanja wa Chuo Kikuu Cha
Ushirika Moshi (MOCU). Ameshauri mbio hizo ziitwe Kilimanjaro
International Marathon kwa kuwa zinashirikisha mataifa mengi duniani.
“Michezo
hii inatusaidia katika kujenga afya, urafiki, kukuza ujasiriamali na
kuimarisha sekta ya utalii. Michezo ni uchumi. Nimefahamishwa kuwa mbio
hizi zimeshirikisha wakimbiaji zaidi ya 12,000 kutoka mataifa zaidi ya
55 duniani. Hii ni idadi kubwa sana na ni faida kubwa kwa nchi yetu
kwani kupitia washiriki wa riadha hao kunawezesha nchi yetu kupata fedha
za kigeni.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi mshindi wa kwanza wa mbio za Kilometa 42 za Kilimanjaro Maarthon (wanaume) , Aloyce Simbu kutoka Tanzania katika maadhimisho ya mika 20 ya Marathon hiyo kwenye uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi, Februari 27, 2022. Kushoto ni mshindi wa pili Amold Kiptaqi wa Kenya na kulia ni mshindi wa tatu, James Tallam kutoka Kenya (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu amesema mbali na
kuimarisha hali ya uchumi, amesema michezo pia inaimarisha afya bora kwa
kushiriki katika mazoezi au shughuli za nguvu kwa ajili ya kujikinga na
maradhi ambayo yamekuwa yakiongeza gharama za matibabu na kupotea kwa
nguvu kazi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya
Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii
zishirikiane na waandaaji wa Kilimanjaro Marathon ili kutangaza zaidi
fursa za utalii na vivutio mbalimbali kwa manufaa ya Taifa. “Kilimanjaro
Marathon ni chapa (Brand) kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo, nina
hakika fursa zake zikitumika vizuri itasaidia kuongeza idadi ya watalii
nchini.”
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia ipitie mitaala ya Elimu Msingi kwa ajili ya kufundisha elimu
kwa michezo na kuanzisha vituo vya michezo (Sports Academy) ili watoto
wenye vipawa waweze kulelewa na kukuza vipawa vyao.
“Hii
itaiwezesha nchi yetu kuwa na wachezaji wenye utaalamu na mahiri ambao
wataweza kuwakilisha vema Taifa letu kwenye medani za kimataifa. Suala
hili lipewe kipaumbele kwani sote tunatambua kuwa michezo ni zaidi ya
burudani na inao uwezo wa kutoa ajira ndani na nje ya nchi.”
“Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi zetu
ione uwezekano wa kupatikana kwa fursa za kusomesha walimu wa michezo
watakaosaidia kunoa timu zetu. Wakati umefika suala la michezo
lichukuliwe uzito unaostahili kwani pamoja na mambo mengine michezo inao
uwezo mkubwa wa kuinua pato la Taifa letu.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wadhamini, viongozi pamoja na washindi watatu wa mbio za Kilimanjaro Marathon za Kilomita 42, (wanaume) baada ya kuwakabidhi zawadi zao kwenye uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi, Februari 27, 2022. Viongozi hao ni Naibu Waziri wa maliasili na Utalii, Mary Masanja, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bia Tanzani (TBL), Jose Dmoran na kulia ni Naibu Waziri waUtamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul. Washindi hao (mstari wa nyuma) ni mshindi wa kwanza, Aloyce Simbu wa Tanzania,(katikati, Mshindi wa pili Amold Kiptaqi wa Kenya (kushoto) na kulia ni mshindi wa tatu James Tallam wa Kenya. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Amesema uwepo wa mchezo huo wa riadha ni fursa nzuri ya kuendeleza utalii wa michezo yaani ‘sport tourism’. “Washiriki wa mchezo huu pamoja na riadha wanapata fursa ya kufanya utalii katika vivutio vyetu mbalimbali kama vile Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro, Zanzibar na maeneo mengine.”
Akizungumzia kuhusu matumizi ya cable cars zitakazotumika kupanda mlima Kilimanjaro, Waziri Mkuu amewataka wahusika wa mradi huo waandae mpango mkakati wa utekelezaji wake ambao utachambua athari za kimazingira pamoja na ajira hususani kwa vijana wengi wanaofanya shughuli za kiutalii kwenye maeneo hayo.
Tags
Michezo