NA MWANDISHI MAALUM
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiongozana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango
leo Februari 20, 2022 wamefika nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu
Samwel Malecela Mtaa wa Kilimani jijini Dodoma kutoa pole kufuatia kifo
cha mtoto wake Dkt. Mwele Ntuli Malecela kilichotokea Februari 10,
2022 jijini Geneva nchini Uswisi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu Samwel Malecela mtaa wa Kilimani Jijini Dodoma alipofika kutoa pole kufuatia kifo cha Dkt. Mwele Ntuli.
Akitoa neno la faraja kwa familia na waombolezaji mbalimbali
waliojitokeza nyumbani hapo, Makamu wa Rais amewasihi kuwa na moyo wa
subira katika kipindi hiki kigumu pamoja na kumuombea marehemu apate
pumziko la Amani.
Makamu wa Rais amemtaja Dkt. Mwele kama shujaa
aliejitoa kupigania Afya za wananchi wengine kupitia tafiti mbalimbali
alizokuwa akizifanya zenye lengo la kusaidia jamii kupambana na magonjwa
mbalimbali. Amesema Dkt. Mwele alifanya kazi iliyo njema na kuonekana
katika jamii ndani na nje ya nchi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitoa neno la faraja kwa familia ya Waziri Mkuu Mstaafu Samwel Malecela pamoja na waombolezaji mbalimbali kufuatia kifo cha Dkt. Mwele Ntuli Malecela mara baada ya kufika nyumbani kwa Malecela mtaa wa Kilimani Jijini Dodoma.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiagana na Waziri Mkuu Mstaafu Samwel Malecela mara baada ya kutoa pole kwa familia na heshima zake za mwisho kwa mwili wa Dkt. Mwele Ntuli aliefariki dunia tarehe 10 Februari 2022 Geneva nchini Uswisi.
Aidha Makamu wa Rais amesema katika kipindi cha uhai wake Dkt. Mwele Malecela aliinua jina la Tanzania kwa kuaminiwa kufanya kazi katika taasisi kubwa ya afya duniani. Amesema uwezo wa Dkt. Mwele katika kazi pia uliinua wanawake hapa nchini hivyo hapana budi kumshukuru Mungu kwa zawadi hiyo pamoja kumuombea ampokee ili apumzike kwa Amani.
Tags
Habari