Picha mbalimbali zikionesha namna ambavyo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali leo Februari 22, 2022 walikuwa wakijiandaa kwenda kuteketeza jumla ya kilo 250.7 za dawa za kulevya zikijumuisha kilo 51.7 za heroine na kilo 199 zenye mchanganyiko wa heroine na cocaine katika kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara.
Uteketezaji huu ni kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mahakama iliyotolewa katika kesi Namba 2 ya Mwaka 2018 kwenye kikao cha Mahakama Kuu kilichoketi mwishoni mwa mwezi Oktoba na kumalizika tarehe 5 Novemba 2021 mkoani Lindi mbele ya Jaji Latifa Mansour.
Kesi hiyo iliwahusisha washtakiwa Sano Sidiki na Tukure Ally ambao wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kila mmoja.
Amri nyingine ya uteketezaji ilitolewa na Mheshimiwa Jaji Isaya Arufan tarehe 29 Novemba, 2021 kwenye kesi Namba 25 ya mwaka 2019 iliyowahusisha washtakiwa Mohamed Nyamvi na Ahmad Said Mohamed. Katika kesi hiyo washtakiwa hao walihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 kila mmoja.
Zoezi hilo limefanyika kwa mujibu wa Kanuni Namba 14 ya Kanuni za Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya za mwaka 2016 za Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015.
Kanuni hiyo inaelekeza kuteketeza dawa za kulevya baada ya shauri kumalizika Mahakamani na kwa dawa za kulevya zenye tabia ya kubadilika au kuharibika endapo zitakaa kwa muda mrefu uteketezaji wake unaweza kufanyika kabla au wakati shauri husika linaendelea kusikilizwa Mahakamani.
Uteketezaji huu umefanyika kwa uwazi mbele ya wadau wote muhimu wanaotambulika kisheria na kushuhudiwa na waandishi wa habari ili kuondoa dhana iliyojengeka kwa baadhi ya wananchi kwamba, baada ya dawa za kulevya kukamatwa kurejeshwa mtaani na kuuzwa tena.