NA FRESHA KINASA
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Mjini Mh. Vedastus Mathayo (CCM) ameahidi kufanya ukarabati wa mfumo wa umeme ambao umechakaa katika mabweni ya wasichana Shule ya Sekondari ya Wasichana Songe iliyopo Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara kufuatia kilio cha uchakavu wa mfumo wa umeme katika mabweni na baadhi ya majengo kubainishwa na mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Rosemary John.
Mheshimiwa Mathayo ametoa ahadi hiyo Februari 24, 2022 wakati akizungumza na wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo kwa njia ya simu Kupitia Mwenyekiti wa Wazazi wa Shule hiyo George Marato katika kikao chao cha pamoja kilichofanyika shuleni hapo kujadiliana mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta ya elimu ambapo wazazi wamekubalina kila mmoja kuchangia shilingi elfu 50,000, kusaidia ujenzi wa bweni la wasichana, Shilingi 10,000 kila mzazi motisha ya walimu pamoja na rimu moja kila mzazi.
Kabla ya Mheshimiwa Mbunge kutoa kauli hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Songe Rosemary John alisema kuwa, shule hiyo inakabikiwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu ya maji, majengo na mifumo ya umeme katika majengo ya shule hiyo kwani asilimia kubwa miundombinu yake imechakaa na wakati mwingine kuhatarisha usalama.
"Nimesikia kuna kilio cha uchakavu wa mbweni mengi hapo shuleni Songe. Mimi nitaanza na hili la umeme shuleni hapo. nitamtuma mtu wangu fundi (umeme) kuja kuangalia nini kinahitajika ikiwemo gharama ili wiki ijayo kazi hiyo ya marekebosho ianze mara moja. Sitaishia hapo tu, nitakuja mwenyewe pia shuleni hapo kuangalia changamoto mbalimbali na kuona namna ya kuzitatua ili watoto wasome kwa ufanisi wafikie ndoto zao,"alisema Mheshimiwa Mathayo kupitia simu huku akishangiliwa na wazazi.
Mwalimu Rosemary alisema kuwa, majengo mengi ya shule hiyo yamechakaa sana na mfumo wa umeme umechakaa unahitaji marekebisho makubwa kwa ajili ya usalama wa watoto.
Akasema tayari suala hilo linafahamika na uongozi wa Manispaa ya Musoma kupitia Mkurugenzi wake ambaye pia alituma timu ikaja shuleni hapo na kujiridhisha na uchakavu huo na hatua kadhaa ikiwemo kukarabati mfumo wa umeme katika jengo moja wapo shuleni hapo umefanyika.
"Mkurugenzi alisaidia kusuka jengo moja mfumo wake ulikuwa umechakaa Sana, sisi Kama shule tuneendelea kurekebisha kidogo kidogo jengo moja moja kulingana na upatikanaji wa fedha zinazotolewa na serikali kusaidia elimu bure, ukweli ni kwamba, miundombinu ya umeme inahitaji marekebisho makubwa kukabiliana na majanga ya shoti ya umeme," amesema Rosemary John.
Aidha, changamoto nyingine Rosemary alisema, ni ukosefu wa usafiri shuleni hapo hasa wanapougua nyakati za usiku, ukosefu wa maktaba, upungifu wa watumishi pamoja na mabweni akaomba wadau mbalimbali kusaidia kuondoa changamoto hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wazazi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe, George Marato, amewahimiza wazazi na walezi wote kujitahidi kuwatimizia mahitaji yao watoto wanapokuja shuleni, hatua ambayo itawafanya wasome kwa ufanisi sambamba na kufuatilia kwa Karibu Maendeleo yao kitaaluma kwa kuwa na mawasiliano ya karibu na Waalimu.
Marato, amewahimiza wazazi na walezi kuwa na utaratibu wa kupiga simu kwa walimu kuulizia maendeleo ya watoto wao na ikibidi kufika shuleni kuulizia maendeleo ya watoto wao sambamba na kushirikiana pamoja na serikali. Huku pia akiwagimiza Wazazi kuwakatia bima ya afya Watoto wao kwa ajili ya uhakika wa matibabu pindi wanapougua.
Afisa Elimu Manispaa ya Musoma Avith Mallya amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanashiriki vyema kuchochea ufaulu wa Watoto wao badala ya kuiachia jukumu hilo serikali pekee, amesema kila mzazi ananafasi kwa sehemu yake ,huku akisema mkakati uliowekwa ni kuwa na matokeo bora kwa wanafunzi wote kwa kupata daraja la kwanza, la pili na la tatu
Ameongeza kuwa, katika kuinua ufaulu wa wanafunzi Manispaa ya Musoma imeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba walimu wanafundisha silabasi zote zinaisha kwa wakati na mitihani ya mihura inatungwa na Walimu wengine na kufanywa na wanafunzi wote wa Manispaa ya Musoma ili Kama kuna somo halijafanya vizuri iwe rahisi kufanya ufuatiliaji kwa somo husika na shule husika badala ya kila shule kutunga mtihani wake.
Awali akitoa taarifa ya Maendeleo ya taaluma shuleni hapo Mwalimu Charles Bwire alisema kuwa shule hiyo inawanafunzi 495 kuanzia kidato cha kwanza hadi Cha sita, na matokeo ya kidato Cha nne kwa mwaka 2021 wanafunzi 80 walifanya mtihani ambapo daraja la kwanza walipata wanafunzi 28, daraja la pili wanafunzi 23, daraja la tatu wanafunzi 19, na daraja la nne wanafunzi 10. daraja 0 halikuwepo.
Kwa upande wa matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka 2021 jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 41, ambapo waliopata daraja la kwanza walikuwa 34, daraja la pili wanafunzi 6, na daraja la tatu wanafunzi 1, na daraja la nne 0.
Ivon Gerrard ni Mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyefanya vizuri katika mtihani wa kidato pili na kupata daraja la kwanza pointi Saba, ambapo amesema, anaamini wanafunzi wote wataendelea kufanya vizuri katika mitihani yao kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Walimu kufundisha kwa bidii pamoja na wanafunzi kuzingatia masomo na nidhamu.
Juma Peter na Paul Joshua ni Wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ambapo wamepongeza uamzi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini Vedastus Mathayo Manyinyi kujitolea kufanya ukarabati wa mfumo wa umeme katika mabweni ya shule hiyo Jambo ambalo linalinda usalama wa watoto.
Katika kikao hicho Cha Wazazi na walezi, wameendesha zoezi la mchango wa hiari na kuwapa fedha wanafunzi 12 waliofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha pili kuingia kidato cha tatu.