Mbunge Neema Lugangira: TBS kwa usalama wa chakula hapana

NA GODFREY NNKO

MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania (NGOs),Mheshimiwa Neema Lugangira ameonesha kutoridhishwa na uamuzi wa Serikali kulipa jukumu la kuratibu na kudhibiti usalama wa chakula Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hatua ambayo amesema ni sawa na kuyaweka maisha ya Watanzania rehani.
Ameyasema hayo leo Februari 11, 2022 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hoja katika Taarifa ya Mwaka ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Mheshimiwa Lugangira ambaye amejikita katika suala la usalama wa chakula amesema kuwa, masuala yote yanayohusiana na mambo ya chakula duniani kote huwa yanaratibiwa chini ya Wizara ya Afya ili kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama muda wote. 

"Ninajikita katika suala la usalama wa chakula kwa maana ya 'food safety', ninasema hivi mheshimiwa Naibu Spika kwa sababu Duniani kote masuala mazima ya chakula yanaratibiwa chini ya Wizara ya Afya. Kwa maana ya kuwa chini ya Mamlaka ya Kudhibiti ubora wa Chakula na Dawa. 

"Na hata Tanzania miaka ya nyuma ndivyo ambavyo tulikuwa tukifanya, chini ya TFDA, na hata nchi za Afrika Mashariki zilikuja kwetu kuja kujifunza. Lakini, miaka ya karibuni Serikali iliamua kuivunja TFDA na badala yake kuunda TMDA, na jukumu la usalama wa chakula kwa maana ya food safety wakaliweka chini ya Shirika la Viwango (TBS). 

"Sasa jambo hili, limeweka maisha na afya za Watanzania rehani. Ninasema hivyo kwa sababu, TBS ina jukumu la kuangalia ubora wa matairi, ubora wa mabati, ubora wa misumari na kadhalika. Na hapo hapo iweje TBS hiyo hiyo ipewe jukumu la kuratibu na kudhibiti usalama wa chakula? Na hawa hawa TBS ndiyo wanaotoa vibali kwa wazalishaji wa vyakula, halafu hao hao tena waende waangalie kama kile kibali walichotoa kinakidhi ubora, tayari hapo kuna conflict of interests (mgongano wa maslahi),"amefafanua Mheshimiwa Lugangira.

Mbunge huyo amesisitiza kuwa, TBS wanapaswa kuendelea kudhibiti ubora wa mambo mengine na yasiyoendana kabisa na usalama wa chakula.

Tulikotoka

Hoja ya Mheshimiwa Lugangira inajiri ikiwa, jukumu la kudhibiti chakula na vipodozi lilihamishwa kutoka iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kwenda Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Hatua hiyo ilikuja kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura ya 219 yaliyofanyika kupitia mabadiliko ya mfumo wa sheria ambayo yalifanywa kupitia Sheria ya Fedha, Namba 8 ya 2019 ambayo pia yalisababisha kubadilishwa kwa jina na kuwa TMDA.

Kufuatia mabadiliko hayo iliyokuwa TFDA kwa sasa, inatambulika kama Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ikiwa na jukumu la kudhibiti dawa, tiba na vitendanishi nchini.

Aidha TMDA imeainisha baadhi ya majukumu ambayo yatakuwa yakitolewa na TBS, ikiwa ni pamoja na kupokea maombi na usajili wa bidhaa zote za chakula na vipodozi zinazotengenezwa hapa nchini au vile vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi.

Majukumu mengine ni kufanya ukaguzi wa maeneo yote yanayojihusisha na utengenezaji, utunzaji, usambazaji na uuzaji wa chakula na vipodozi.

Mbali na hayo pia itatoa vibali vya uingizaji nchini na usafirishaji nje ya nchi, kwa bidhaa zote za chakula na vipodozi ikiwa ni pamoja na ukaguzi kwenye vituo vya forodha.

Kwa nini Mheshimiwa anasema hivyo?

"Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo mahususi ambalo lilitokea likadhirisha wazi kuwa TBS haiwezi kuendelea kubeba jukumu la usalama wa chakula, mwaka jana mwezi wa 10, kwenye tarehe 13, 14 Oktoba, 2021. Shirika la Chakula na Madawa la Kenya lilitangaza kwamba linarudisha juisi aina ya cereals za Apple ambazo zilikuwa na aina moja ya sumu kuvu ambayo ni hatari kwa maisha ya wanadamu.

"Mpaka siku hiyo, kwa huku Tanzania, TBS ilikuwa haijasema kitu chochote, gazeti la Mwananchi likawatafuta TBS, nakumbuka Mkurugenzi mwenye idara husika alisema kwamba, mpaka muda ule wa tarehe 14, mwezi wa 10, juisi aina ya cereals zilikuwa hazijaingia nchini, na wanaendelea kufuatilia, na pale ambapo zitaingia nchini, basi watazizuia, na watatoa taarifa na watafanya uchunguzi.

"Siku ya tarehe 16, Oktoba...TBS wakatoa taarifa kwa umma, kuelezea kwamba, wamejiridhisha kwamba, juisi zile hazijaingia nchini, juisi aina ya cereals na barcode ambazo zilikuwa zimewekwa, wakauambia umma kuwa kila kitu kipo sawa, lakini Mheshimiwa Naibu Spika, TBS kwa masikitiko makubwa walitudanganya Watanzania. Kwa sababu kwenye tarehe 22, mimi kwenye kioski kimoja wapo hapa Dodoma nilikuta zile juisi aina ya cereals za Apple zinauzwa. 

"Na nilichukua jukumu la kupiga picha na kumtumia Waziri mwenye dhamana wa wakati ule wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Akapokea na kusema atalifanyia kazi. Kwa hiyo moja kwa moja inaonesha kwamba, kwanza TBS hawalichukulii serious suala la usalama wa chakula. TBS hawana muda wa kuangalia masuala ya usalama wa chakula.

"TBS wanaendelea kuhatarisha maisha ya Watanzania, kwa kuendelea kulimbikiza mambo mengi ambayo hayaendani pia na usalama wa chakula, kwa hiyo kwa unyenyekevu mkubwa Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ipitie upya uamuzi wake wa kuondoa masuala ya usalama wa chakula kutoka Wizara ya Afya na kuyapelekea kwenye eneo la viwanda, biashara na kadhalika,"amefafanua Mheshimiwa Lugangira wakati akichangia hoja bungeni jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news