*Ataka wananchi walipwe fidia, wahamishwe
NA MWANDISHI MAALUM
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CHADEMA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa wa chama hicho, aliyewahi pia kuwa Mbunge wa Iringa Mjini na Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa amesema hali ni mbaya katika Hifadhi ya Ngorongoro na jitihada za haraka kuinusuru hifadhi hiyo zinahitajika huku akiilaumu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutaka kuiuwa hifadhi hiyo.
Mchungaji Msigwa ameishangaa Serikali kwa kushindwa kufanya maamuzi sahihi kwa wakati kuinusuru hifadhi hiyo licha ya kuwa na ongezeko kubwa la watu na mifugo linalohatarisha ustawi wa watu ,wanyama na uhifadhi wa eneo la Ngorongoro kwa kuogopa kupoteza kura za uchaguzi bila kujali maslahi mapana ya taifa na ya eneo husika yanayotokana na shughuli mbalimbali ikiwemo utalii.
“Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inatukosea sana,kama haiwezi kutunza mali ambazo tumewapa,wanatukosea sana,hizi mali ikiwemo Serengeti, Ngorongoro, Mkomazi,Ruaha au Kitulo,hii sio mali ya CCM ni mali ya Taifa kwa hiyo CCM imepewa dhamana ya kutunza, wanapokuwa wazembe kiasi hiki,watu mpaka wanajenga mle ndani,mle ndani wanafuga ng’ombe wanaozidi zaidi maanake wanatukosea sisi na ndio maana tunataka tuwatoe madarakani wanashindwa kutunza mali za umma ambazo wamepewa dhamana wazitunza,"amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa, hali ya watu wa Ngorongoro ni mbaya na ameishauri serikali kutoa fidia itakayowashawishi wakazi hao kuhama kwenda sehemu bora zaidi watakazopatiwa huduma na mahitaji yanayoendana na changamoto za sasa.
Pia amewaasa wasomi wa kabila la kimaasai ambao wanapaza sauti kutokea Dar es Salaam kushinikiza wananchi wanyonge wa Ngorongoro wasibadilishiwe maisha yao kwa kisingizio cha sheria ambayo kimsingi sio msaafu wala biblia na imetokana na matakwa ya kikoloni,kiasi cha kuwazuia wakazi wa eneo hilo kushindwa kujenga nyumba za kisasa, miundombinu bora ya huduma za kijamii.
Pia amewashangaa wabunge waliopita na wa sasa wa eno hilo kuwa mstari wa mbele katika uvunjifu wa sheria wanayoitetea.