NA MWANDISHI MAALUM-WUU
SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imesema ahadi zote zilizotolewa kupitia Ilani, bajeti na maelekezo ya viongozi wa kitaifa za ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja walizozitoa katika ziara mbalimbali nchini zinatekelezwa kwa wakati na ubora ili kusaidia kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na Taifa kwa ujumla.
Muonekano wa Daraja la Msingi (m 100), ambalo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa Wilaya ya Mkalama na Iramba, mkoani Singida. Ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 98 na unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 10.9.
Hayo yamesemwa mkoani Singida na Naibu Waziri wa Wizara hiyo anayesimamia Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alipokuwa akikagua utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la Msingi lenye urefu wa mita 100 na barabara za maingilio zenye urefu wa kilomita moja kwa kiwango cha lami ambao ujenzi wake umefikia asilimia 98.
Naibu Waziri Kasekenya amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo ni moja ya ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kwa wakazi wa mikoa ya Singida na Simiyu na sasa lipo katika hatua za mwisho.
“Nimefika hapa kujionea kazi zinazoendelea na nimeridhika na kazi zilizofikiwa katika daraja hili la msingi ambalo ni kiungo muhimu sana kwa wakazi wa wilaya ya Mkalama na Iramba,”amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na mkandarasi mzawa wa Kampuni ya Gemin Engineering, anayejenga Daraja la msingi (m 100) na barabara za maingilio (km 1), mkoani Singida.
Aidha, Mhandisi Kasekenya amesema kukamilika kwa daraja hilo kutapunguza umbali wa safari kwa kilomita 200 kwa magari yanayopita Singida kuelekea mikoa ya Simiyu na Mara badala ya kupita njia ya Mwanza.
Naibu Waziri Kasekenya ameeleza kuwa madhumuni ya daraja hilo ni pamoja na kuwaondelea wananchi kero ya usafiri wa barabara waliokuwa wanaipata kutokana na daraja la vyuma la zamani lililokuwa la muda kuwa jembamba na kuleta adha ya usafiri na usafirishaji.
Ameongeza kuwa, usanifu wa barabara hiyo ya mkoa inayoanzia Ulemo – Gumanga – Sibiti inaendelea kufanyiwa usanifu wa kina na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida, Mhandisi Matari Masige, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa Daraja la Msingi (m 100), mkoani Singida.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha inaunganisha barabara za mikoa kwa mikoa kwa kiwango cha lami na kwa hii barabara tumekamilisha madaraja makubwa mawili ya Sibiti na Msingi na sasa usanifu wa barabara unaendelea kwa ajili ya kuweka lami,”amefafanua Naibu Waziri huyo.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Singida, Mhandisi Matari Masige, ameeleza kuwa Daraja la Msingi linatekelezwa na mkandarasi mzawa kampuni ya Gemin Engineering kwa gharama ya shilingi Bilioni 10.9 na mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2022.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa daraja hilo unafanyika takribani umbali wa mita 10 upande wa juu toka lilipo daraja la sasa likiwa na urefu wa meta 100 zilizogawanywa sawa katika sehemu nne zenye urefu wa meta 25 kila sehemu.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, akikagua kingo za Daraja la Msingi (m 100), ambao ujenzi wake umefikia asilimia 98, mkoani Singida. Daraja hilo ni kiungo muhimu kwa mkoa wa Singida na Simiyu. (PICHA NA WUU).
Mhandisi Masige amesema kuwa, Daraja hilo lina jumla ya upana wa meta 10.2 zinazojumuhisha upana wa meta 7.6 ikiwa ni sehemu ya njia za kupitisha magari mawili kwa wakati mmoja na sehemu iliyosanifiwa kupita kwa watembea kwa miguu yenye upana wa meta 1.3 kila upande.
“Daraja hili linajengwa kwa zege na litakuwa la kudumu zaidi ya miaka mia moja (100). Pia magari yenye uzito zaidi ya tani 50 yatapita baada ya kukamilika daraja hili hivyo kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwa wingi na hivyo kuinua uchumi kwa wananchi,”amefafanua Mhandisi Masige.
Naye, Mkandarasi kutoka Kampuni ya Gemini Engineering, Man Andrew Nyantori, ameishukuru Serikali kwa kuwaamini wakandarasi wazawa kwa kuwapatia miradi mikubwa na ya kimkakati na kusisitiza kuwa Serikali isiwachoke na iendelee kuwainua kwa ajili ya kupata watalaam wabobezi kwa maslahi ya nchi.
Daraja la Msingi ni kiungo muhimu kati ya Mkoa wa Singida na Mikoa ya Simiyu na Mara kupitia barabara ya Mkoa ya Ulemo – Gumanga – Sibiti ambapo pia inaunganisha makao makuu ya Wilaya ya Mkalama na Wilaya ya Iramba.