NA GEOFREY KAZAULA-TARURA
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff amefanya ziara ya kikazi mkoani Mbeya lengo kubwa likiwa ni kutatua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa miradi miwili.
Miradi hiyo ni ujenzi wa Barabara ya Inyara – Simambwe kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 16.7 na ujenzi wa Barabara ya Lupeta- Wimba- Izumbwe kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 9.5.
Kiongozi huyo amebainisha kuwa kwa mujibu wa mikataba hiyo, miradi yote ilitarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2020, lakini kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza utekelezaji wa miradi hiyo unasuasua.
Akielezea kuhusu mkataba wa barabara ya Inyara -Simambwe uliokuwa unatekelezwa na Mkandarasi Milembe Construction Company Ltd ambao utekelezaji wake upo asilimia 55 ya utekelezaji kiongozi huyo amebainisha kuwa, TARURA imefikia uamuzi wa kuvunja mkataba huo baada ya kufuata taratibu zote na kujiridhisha kuwa Mkandarasi hana uwezo wa kumaliza kazi hiyo kwa wakati.
"TARURA imefikia maamuzi haya baada ya kujiridhisha kuwa, Mkandarasi hawezi kumaliza kazi hii kwa wakati na sasa tayari hatua za manunuzi zimeanza ili kumpata Mkandarasi atakayeweza kukamilisha mradi huu ili utoe huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa,"amesema Mhandisi Seff.
Kuhusu utekelezaji wa mradi wa Lupeta – Wimba- Izumbwe unaotekelezwa na CANOPIES INTERNATIONAL (T) LTD ambapo utekelezaji umefikia asilimia 54, Mkandarasi huyo ameomba ufafanuzi wa baadhi ya sehemu ambazo kulikuwa na udongo usiofaa na pia ameomba kuongezewa muda wa nyongeza wa miezi miwili.
Baada ya ukaguzi wa mradi na kupitia changamoto zote ilikubalika kuwa upimaji wenye maeneo yaliyo na shida ya udongo yafanyike kwa pamoja kati ya Mkandarasi na wataalamu wa TARURA na uchambuzi ufanywe upya ikiwa ni pamoja na kupitia upya maombi ya kuongezewa muda na Mtendaji Mkuu ameagiza kazi hii ikamilike ifikapo Machi 7,2022.
Aidha, Mtendaji Mkuu amefanya kikao na watumishi wakiwemo Mameneja wa TARURA wa wilaya zote tano za Mkoa wa Mbeya na kutoa maelekezo mbalimbali ikiwemo kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi katika maeneo yao na pia kukagua madaraja mara kwa mara na hasa kabla ya mvua kuanza kunyesha ili kuzuia ajali zinazoweza kutokana na kukatika kwa madaraja.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) unaendelea na utekelezaji wa miradi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha barabara zinafunguliwa na kuwafikisha wananchi kufika kusiko fikika.