NA MARY MARGWE
MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka amesema, hatoondoka madarakani kwa kukosa kura bali ataondoka mwenyewe kwa hiari kwa kusoma upepo wa wana Simanjiro.
Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha wadau wa elimu kilichoitishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Dkt.Suleiman Serera, kilichofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Simanjiro, ambapo Bilionea Saniniu Laizer pamoja na mdogo wake Kiria Laizer walikuwa ni moja kati ya wageni walialikwa kwenye kikao hicho.
Mbunge Sendeka amesema, waliokuwa wakisema kuwa yeye hatogombea ubunge mwaka 2025 wanapoteza muda ama wanajifurahisha, watambue kuwa yeye ndiye Mbunge wa jimbo hilo, hivyo 2025 bado atawania tena ubunge wa jimbo hilo.
Aidha, alisema yupo aliyemfuatia kwa kura Mjumbe wa Kamati ya Siasa mkoa ambaye ni Kiria Laizer ( Mdogo wake na Bilionea Saniniu Leizer ambaye alidai ana nguvu na alimfuata kwa kura kwa kushika namba mbili).
"Msimuone hivi huyu Kiria kwenye kura za ubunge yeye ndiye alikuwa namba mbili, kwa hiyo hata akitoa pokeeni tena, mie mwenyewe nimezunguka naye kwenye kampeni ni mdogo wangu ikifika siku akiniangusha kama akitaka kuniangusha, kuna ubaya? Mkimtaka Kiria si hakuna ubaya,"amesema Ole Sendeka.
Aidha, alisema siku itafika tu Ole Sendeka ama atatoka kwa kura au atatoka kwa kuondoka mwenyewe.
"Lakini siku itafika tu Ole Sendeka ama atatoka kwa kura au atatoka kwa kuondoka mwenyewe na mimi nataka niwaambieni sitaondoka kwa kura, nitaondoka mwenyewe kwa hiari kwa kusoma upepo wa wana Simanjiro unapoelekea,"amefafanua Sendeka.