NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuendelea na ujenzi wa miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) iliyokwama.
Miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa iliyokwama Dar es Salaam ni ule wa Kawe na Morocco Square na miradi hiyo ilisimama tangu mwaka 2017 kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za kifedha na mabadiliko ya baadhi ya maboresho kwenye majengo ya Morocco Square.
Naibu Waziri wa Ardhi alieleza hayo Bungeni Februari 9, 2022 wakati akichangia hoja iliyowasilishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
“Serikali iko tayari kukamilisha miradi iliyokuwa imesimama inayojengwa katika Kiwanja No.300 Regent Estate, Kiwanja No. 711, na Moroco Square,"amesema Ridhiwani Kikwete.
Amesema, Serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha miradi ya NHC iliyokwama inakamilika ili iweze kukaa vizuri na katika hatua ilizofanya Shirika la Nyumba la Taifa ni kuomba kuchukua fedha kutoka vyanzo vyake vingine au kukopa katika taasisi za fedha li kukamilisha miradi iliyokwama.
Hata hivyo, Ridhiwani aliwaambia wabunge kuwa, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan Serikali ilielekeza kamati inayosimamia madeni iangalie vizuri yale yaliyoombwa na NHC ambapo katika kuchakata kwake liliruhusiwa shirika kukopa shilingi bilioni 44.7 ili kukamilisha miradi hiyo.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 19 zinaenda plot 300 na kiasi kilichobaki kiende kwenye mradi wa Morocco Square. Hata hivyo, kuhusu eneo la Kawe maelekezo ni kuwa Shirika likae na Mwekezaji Mwenza Kampuni ya Al-Gurey-Dubai kuona namna bora ya kuendelea na mradi wa eneo hilo.
Naibu Waziri Ridhiwani alisema, baada ya mazungumzo na Mwekezaji Mwenza hatua iliyofikiwa baada ya mikutano mitatu ni kwamba mbia anaenda kuwasiliana na wenzake ili mambo watakayokubaliwa basi waje kuzungumza kwa pamoja.