Miaka 45 ya CCM, Shaka aanika mafanikio yaliyopatikana

NA FRESHA KINASA

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa, katika kipindi cha miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM, chama hicho kimeendelea na harakati za kuleta maendeleo nchini pamoja na kudumisha amani na Muungano uliopo kutokana na juhudi za makusudi za chama hicho katika kutatua changamoto za Muungano kwa masilahi mapana ya Watanzania.
Ameyasema hayo leo Februari 4, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Mkoa wa Mara yaliyopo Mjini Musoma wakati akielezea mafanikio mbalimbali yaliyopatikana nchini chini ya chama hicho. 

Amesema, mafanikio yaliyopatikana ni mengi na hayawezi kuelezeka kwa muda mfupi, miongoni mwake ni pamoja na kudumisha umoja wa Kitaifa, kukuza demokrasia,  kuleta maendeleo kwa wananchi na kutoa fundisho na somo kwa Afrika kutokana na kuaminika zaidi. 

Katika maadhimisho hayo ya miaka 45 ambayo yanafanyika tarehe 5/2/2022, Shaka amesema Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan atazindua zoezi la utoaji wa kadi za kielektroniki ambazo zitakuwa na fursa mbalimbali kwa wanachama wa chama hicho huku akibainisha kuwa maadhimisho hayo yamefanyika mkoani Mara kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius kambarage Nyerere na kuadhimisha miaka 100 ya Mwalimu Nyerere.

"Tunamshukuru Rais Samia kuendelea kudumisha Muungano, umoja na amani iliyopo nchini mbali na utofauti wa Kisiasa tulionao tumetanguliza mbele utaifa wetu jambo ambalo ni nadra katika nchi nyingine ambazo zimekuwa zikitetereka katika suala zima la amani," amesema Shaka.
Shaka ameongeza kuwa, wananchi wameendelea kuvumiliana na kuthaminiana licha ya utofauti wa Kisiasa nchini ambapo chama pia kimeendelea kuimarisha hali ya maisha ya Watanzania na kuendelea kuwa katika hali nzuri, kwani tangu mwaka 1977 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi barabara, umeme, na maendeleo mengine pamoja na huduma za kijamii zimeimarika. 

Amesema,  miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi imekuwa Mwalimu wa demokrasia nchini ambapo Watanzania wamekuwa wakichagua viongozi kwa njia ya amani. Pamoja na kudumisha ujirani mwema na kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa vyama vingine kwa manufaa ya Watanzania.

Amevihimiza vyama vingine nchini, kuendeleza kudumisha amani na umoja wa Kitaifa nchini na kutotumika kuleta mgawanyiko ambao unaweza kudhoofisha umoja na mshikamano uliopo ambao ndio msingi na chachu kubwa ya maendeleo ya nchi.
Amesema, maendeleo yamepatikana ya kiuchumi, kijamii, na Kisiasa na hivyo chama kitaendeleza mema waliyoyarithi kutoka TANU na ASP huku akishukuru pia kazi nzuri zilizofanywa na Rais Samia tangu alipoingia madarakani ambapo ameonesha dhamira yake ya kuleta Maendeleo kwa Watanzania na kusimama vyema ilani inayotekelezwa na Chama Cha Mapinduzi kwa kiwango na mafanikio na kuendelea kuaminika kwa Watanzania.

Ameongeza kuwa, chama hicho kimeendelea kuwa chama kiongozi kwa kuwa na mafanikio makubwa ya kiuchumi kwa kumudu kujiendesha pamoja na kutengeneza viongozi bora waliolivusha Taifa hadi hapa lilipo na amesema kitaendelea kutoa huduma za msingi na kijamii kwa Watanzania wote bila upendeleo.

Shaka amewataka wakazi wote wa Mkoa wa Mara na Watanzania wote kuhudhuria kwa wingi katika maadhimisho hayo yatakayofanyika Uwanja wa Karume Mjini Musoma ambapo pia yatafanyika matembezi ya mshikamano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news