NA MOHAMED HAMAD
MKUU wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Mbaraka Al-Haji Batenga amesitisha safari ya matofali ya saruji zinazotolewa Babati zaidi ya kilomita 200 hadi kufika Kiteto kwa ajili ya ujenzi wa tenki la maji la lita 300,000.
Tenki hilo linajengwa Kata ya Kaloleni kuondoa adha ya muda mrefu ya maji kwa wananchi ambapo hadi sasa hawapati maji safi na salama kwa zaidi ya asilimia 50.
Ujenzi huo unatokana na fedha za UVIKO-19 ambapo kiasi cha Shilingi Milioni 400 zitatumika kuondoa adha ya maji kwa wananchi wa Kata ya Kaloleni na viunga vyake ambapo hawapati maji safi na salama kwa wakati.
"Hili halikubaliki hata kidogo, hivi Kiteto hatuwezi kufyetua tofali mpaka zitoke huko Babati mkoani Manyara... hapana? Siwezi kukubaliana na haya sasa naagiza Mhandisi, wewe Mkurugenzi wa Wilaya na Mimi tukae pamoja tuone namna ya kupata tofali hizo sio zitoke Babati huko kuja Kiteto mbali sana na ni gharama,"amesema.
Aidha, Batenga alidai Kiteto kuna fursa nyingi, kuna mashine tatu za kufyetulia tofali na ambazo hazina tofauti na tofali zinazoletwa Babati kwanini tusitumie mashine hizo, na wakati huu wa mvua magari yanaweza kushindwa kufika kwa wakati mradi ukasimama.
Akizungumzia zuio hilo, Mhandisi wa Mamlaka ya Maji ya RUWASA, Stephano Mbaruku amekiri tofali hizo kutoka Babati akisema wataongea na mkandarasi ili tofali zitengenezwe Kiteto kuepuka gharama.
Amesema, mamlaka ya maji Kiteto itafuatilia agizo hilo la Mkuu wa Wilaya na maelekezo yake ambayo yataokoa fedha nyingi na ambazo zitaendelea kuwanufaisha wananchi.