NA FRESHA KINASA
ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Jimbo la Bunda na Waziri aliyehudumu katika wizara mbalimbali katika Serikali ya Tanzania, Mheshimiwa Stephen Masatu Wassira amewataka wenye joto na nia ya kugombea nafasi ya Urais kuacha mara moja.
Wassira amesema, Rais aliyepo madarakani hapingwi hadi kipindi cha muda wake wa miaka 10 unapomalizika na kutoa nafasi ya kuteuliwa kugombea nafasi hiyo ndani ya chama hicho.
Mzee Wassira amesisitiza aungwe mkono Rais Samia Suluhu Hassan kusudi aendelee kuchapa kazi ili kuwaletea maendeleo Watanzania kutokana na uchapakazi wake mahiri.
Ameyasema hayo Februari 7, 2022 alipopata wasaa wa kuzungumza katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Miundombinu ya kusafisha maji na kutibu maji (chujio) unaogharimu Bilioni 10.6 Katika Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara, shughuli ambayo imefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amehitimisha rasmi ziara ya kiserikali ya siku nne mkoani humo.
Wassira amesema, Rais Samia ni kiongozi aliyejipambanua, mchapa kazi, mzalendo na mwadilifu wa kweli hivyo aungwe mkono na kila mmoja. Huku akisisitiza kwamba Rais Samia anamuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere kwa vitendo kwa kutekeleza miradi mikubwa na ya kimkakati katika Mkoa wa Mara.
Miradi hiyo ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere katika Manispaa ya Musoma ambayo itakuwa ikitoa matibabu ya kibingwa kwa wakazi wa Mara na maeneo jirani na ujenzi wa Chuo cha Kilimo Butiama sambamba na utekelezaji wa miradi maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Wassira amemuomba Rais Samia pia kuona namna ya kuwezesha ujenzi wa Bandari ya Musoma ambayo itakuwa na faida kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Musoma, Mara na Taifa kwa ujumla.