NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa maana ya Jeshi la Polisi wamefanikiwa kuzima jaribio la kuuza nyumba ya shirika katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.
Biashara hiyo ilikuwa inafanyika Februari 20, 2022 baada ya dalali kutoa taarifa kupitia mtandao kuwa, nyumba hiyo kitalu namba mbili iliyopo katika nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa inauzwa.
Meneja wa Huduma na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Muungano Saguya ameyasema hayo leo Februari 21, 2022 katika eneo la Ubungo zilipo nyumba za shirika wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema, kila jaribio ambalo limepangwa kutendeka dhidi ya nyumba za shirika halitafanikiwa kwa sababu wana kikosi maalum kinachoshirikiana na mamlaka zingine saa 24 kwa ajili ya usimamizi wa nyumba zote nchini.
"Jana katika eneo hili ambalo tupo, ni nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa eneo la Ubungo, tuliweza kuzima jaribio la mpangaji aliyetaka kujaribu kuuza nyumba ya shirika, tulipata taarifa kupitia taarifa iliyotumwa kwa njia ya mtandao na dalali akisema kwamba anauza nyumba ya shirika hapa plot (kitalu) namba 2 ya Shirika la Nyumba hapa Ubungo na baada ya kuona mawasiliano kwa sababu aliweka namba za simu, maafisa wetu wa shirika wa Idara ya Estates, waliweza kufuatilia na kuweza kuweka mtego kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, wakaja hadi hapa.
"Baada ya kufika hapa (Ubungo), waliweza kuwapigia simu kwa maana kwamba wao ni wanunuzi,wakafika. Mwenye nyumba akafika na dalali akafika, wakazungumza bei ya shilingi milioni nane, lakini waka-bargain (kufanya makubaliano) hadi ikafika milioni saba. Sasa baada ya kupata taarifa hiyo na Jeshi la Polisi lilikuwa limeweka kumbukumbu zake kwa maana ya kurekodi, wakajitambulisha kwamba ni maafisa wa Jeshi la Polisi.
"Kwa hiyo watu hao wameshakamatwa na Jeshi la Polisi, na wanaendelea kufanyiwa kazi, na leo watafikishwa kituo cha polisi kwa ajili ya kuandika maelezo. Na hatimaye kuweza kufuata taratibu za kimashtaka kwa sababu walikuwa wanauza nyumba ya shirika ambayo ni mali ya Watanzania,"ameeleza.
Ameendelea kutoa wito kwa Watanzania na wasamaria wema kuendelea kutoa taarifa dhidi ya watu ambao wanakusudia kuuza nyumba za shirika ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Pia Bw.Saguya ameongeza kuwa,pale ambapo mtoa taarifa kuhusu mpango wa kuuza au kuzifanyia hujuma nyumba za shirika, taarifa zake zitakapofanyiwa uchunguzi na kuthibitika kuwa kuna ukweli wowote, shirika hilo litampatia zawadi maalumu ikiwemo yeye kupangishiwa nyumba hiyo.
"Wapangaji kwa wapangaji wamekuwa si waaminifu, wamekuwa wakitafuta watu wengine kwa kutumia madalali na kuuza nyumba za shirika. Kama tulivyokwisha kuwaambia hao ni Watanzania wachache ambao wanajinufaisha na nyumba za shirika ambazo kimsingi ni mali ya Watanzania.
"Tumekuwa tukiendesha zoezi la uhakiki wa wapangaji kujua nani ni nani katika nyumba zetu za shirika. Na tumeweza kuwakamata wapangaji 30 wasiokuwa waaminifu katika nyumba zetu tangu mwaka jana. Kwa kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa maana ya Jeshi la Polisi. Hao watu tumewaondoa katika nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa na kuwapatia Watanzania wengine ambao ni waaminifu,"amefafanua Bw.Saguya.
Wengine wanasemaje?
Kwa nyakati tofauti baadhi ya wapangaji wameonesha kusikitishwa na baadhi ya wenzao ambao si waaminifu, kwa kutumia nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa kuzifanya kama zao jambo ambalo haliwezi kukubalika.
Wakizungumza na DIRAMAKINI kwa nyakati tofauti eneo la tukio wamesema kuwa, vitendo vya namna hiyo ambavyo vinafikia hatua hadi kutaka kuuza nyumba za shirika havipaswi kuungwa mkono kwa sababu ni sehemu ya hujuma kwa mali za umma.
"Hizi nyumba , sisi ni wapangaji tu. Hatuna uhalali wa kuziuza wala kuziharibu, kwani hii si mali ya mtu binafsi, ni mali ya Watanzania, kwa maana hiyo kama ni mali ya Watanzania, sisi wachache ambao tumeaminiwa na kupewa nafasi ya kuja kupanga huku ili kuishi na familia zetu tunapaswa kuziheshimu.
"Tuache kasumba ya ubinafsi na umimi, mfano huyo mpangaji mwezetu yeye katanguliza ubinafsi na roho mbaya kwa mali ya umma, anataka kuiuza mali ya umma kwa maslahi yake mwenye, hilo ni jambo ambalo halikubaliki na halipaswi kuungwa mkono kwa namna yoyote ile. Haya mambo tunayakataa na tunayalaani kwa nguvu zote.
"Kwa sababu ndugu mwandishi, huyo anapofanya hivyo, hapa tunaonekana wote tuna tabia za namna hiyo,ni jambo la kusikitisha sana.Hapa ninakosa cha kusema sana kwa sababu, pengine tungekuwa na utaratibu wa kufahamishana kila kinachojiri kwa mpangaji hapa tungepata taarifa mapema, na hii nyumba ningesikia mimi kwamba inauzwa, ningeonekana mbeya, mara moja ningetoa taarifa kwa uongozi wa shirika, bora uonekane adui kwa wachache, lakini uwe baraka kwa wengi,"amefafanua mmoja wa wapangaji katika nyumba hizo wakati wa mahojiano maalum na DIRAMAKINI.
Dalali anasemaje?
Kwa upande wake dalali (pichani) ambaye anadaiwa kuhusika kutafuta mteja kwa ajili ya kuuziwa nyumba hiyo amesema kuwa, yeye baada ya kudokezwa na muuzaji wa nyumba kuwa ana nyumba eneo la Shekilango (Ubungo) alitangaza kwa usiku mmoja na asubuhi yake akapata wateja wengi.
"Sikujua kama hizi nyumba hazitakiwi kuuzwa, hilo kwa kweli mimi kwangu nilikuwa sijui? Lakini mimi nikipata nyumba lazima nihakikishe mmiliki ananipa documents zake,nipitie, kitambulisho chake nijue kwamba yeye ni mmiliki, lakini kwa hii walisema wanamjua muhusika. Nikafanye hivyo, kwa kweli watu waliitikia wengi kwa sababu watu wana uhitaji na hizi nyumba.
"Nimetangaza usiku na asubuhi wateja wakajitokeza, hii ni nyumba yangu ya kwanza kwa shirika, sijawahi kuuza kabisa,"amesema dalali huyo.
Aliyetaka kuuza
Aidha, mpangaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) aliyetaka kuuza nyumba hiyo (pichani) anaonekana kujutia kufanya uamuzi huo ambao kwa kina tutazidi kukujuza taarifa zake kadri Jeshi la Polisi litakapokalimisha taratibu zake kwa hatua zaidi.