NA MWANDISHI MAALUM-NHIF
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umetakiwa kuimarisha misingi ya kulinda uhai wake na kuwafikia wananchi wengi zaidi ili waweze kunufaika na huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.
Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea Makao Makuu ya Mfuko na kuzungumza na Menejimenti ya Mfuko juu ya utoaji wa huduma zake kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
Alisisitiza upanuaji wa wigo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi ili wawe kwenye utaratibu wa bima ya afya kwa kuwa ni muhimu kwa kila mtu. “Ongezeni jitihada ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuwa na bima ya afya kabla ya kuugua hii itasaidia sana wao kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu," alisema.
“Wekeni mikakati mbalimbali ya kuelimisha wananchi kuelewa dhana ya bima ya afya na kuona umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kwa usalama wa afya zao, tujue Mfuko huu una msaada mkubwa sana kwa wananchi hivyo toeni elimu na muwafikie wananchi huko waliko,” alisisitiza Mhe. Ummy.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri aliagiza uimarishwaji wa mifumo ya TEHAMA ili kuondoa mianya ya vitendo vya udanganyifu. Lakini pia kufanya uwekezaji wenye manufaa kwa Mfuko na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa wakati.