Nigeria yaipongeza Tanzania kwa mazingira bora ya uwekezaji

NA MWANDISHI MAALUM

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango leo Februari 27,2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Nigeria, Prof. Yemi Osinbajo, mazungumzo yaliofanyika jijini Arusha.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amemkaribisha Prof.Osinbajo nchini Tanzania na kuishukuru nchi ya Nigeria kwa ushirikiano uliopo na Tanzania tangu enzi za kupigania uhuru wa nchi za Afrika.

Amesema nchi ya Tanzania na Nigeria zimeendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta za kifedha kupitia United Bank of Africa pamoja na uwekezaji ikiwemo kampuni ya uzalishaji Saruji ya Dangote inayozalisha saruji kwaajili ya Tanzania na nchi jirani.

Dkt. Mpango amemueleza Makamu wa Rais wa Nigeria kwamba nchi hizi mbili bado zina nafasi ya kushirikiana katika masuala mengi zaidi na kumueleza ipo haja ya kuanzishwa kwa tume ya pamoja ya ushirikiano itakayoharakisha ushirikiano katika biashara, utalii, elimu pamoja kushughulikia changamoto mbalimbali zikiwemo za kodi.

Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema Tanzania inaendelea na jitihada za kufufua uchumi uliothiriwa na UVIKO-19 katika sekta mbalimbali.

Amesema serikali inayoongozwa na Rais samia Suluhu Hassan inaendeleza miradi mikubwa ilioasisiwa na Awamu ya Tano ikiwemo ya nishati katika Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) na miundombinu ikiwemo Reli ya kisasa (SGR) pamoja na kuanzisha miradi mipya itakayoimarisha uchumi pamoja na kuboresha maisha ya wananchi.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Nigeria Prof. Yemi Osinbajo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kupokea uwekezaji kutoka nchini Nigeria na kuweka mazingira bora ya ufanyaji biashara kwa wawekezaji hao. 

Amesema, ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Nigeria ni wakindugu ulioanza muda mrefu tangu 1962 ulipoanzishwa ubalozi wa Nigeria Nchini Tanzania.
Aidha, Prof Osinbajo ameongeza kwamba kinachohitajika kwa sasa ni kufanya kazi pamoja, kujivunia rasilimali zilizopo na kwa kutumia viongozi imara waliopo madarakani katika kujiletea maendeleo.

Amesema, Serikali ya Nigeria katika kuimarisha ushirikiano na Tanzania itafuatilia makubaliano yoyote yaliokwama baina ya nchi hizi mbili ili kupata ufumbuzi wa haraka. Ameongeza kwamba, nchi hizi mbili zinapaswa kushirikiana kuliko ilivyo sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news