NA GODFREY NNKO
OFISI ya Waziri Mkuu imetoa maelekezo kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji zikiwemo za Mitaa katika mikoa mbalimbali nchini, ambazo ndizo zenye jukumu la msingi la menejimenti ya maafa, kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara yoyote yanayoweza kujitokeza.
Sambamba na kujiandaa kukabili maafa endapo yatatokea na kurejesha hali kuwa bora zaidi ya ile ya awali wakati wa mvua za masika.
Hayo yamesemwa leo Februari 24,2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu, Mhe.Balozi Dkt. Pindi Chana wakati akitoa tamko la Serikali mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu hatua za kuchukua wakati wa mvua za masika.
Balozi Dkt.Chana amesema kuwa, taarifa ya utabiri wa mwelekeo wa Msimu wa Masika katika kipindi cha Machi hadi Mei, 2022 iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaonesha mvua hizo zitakuwa juu ya wastani katika maeneo mengi ya nchi.
Amesema, kutokana na hali hiyo, imeonekana kuna haja ya Serikali na wadau kuchukua hatua stahiki kuhakikisha matumizi bora ya mvua hizo pamoja na hatua za kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea.
Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt.Chana amesema kuwa, pia utabiri uliotolewa ni mahususi kwa maeneo ambayo hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ambayo ni Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Pia Ukanda wa Pwani ya Kaskazini katika mikoa ya Pwani, Dar es salaam na Tanga, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, visiwa vya Mafia pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Ukanda wa ziwa Victoria Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Waziri amesema,mvua za masika zitarajiwa kuanza mapema kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Februari na kuisha mwezi Mei, 2022 katika maeneo mengi ya nchi.
"Ili kutekeleza agizo hili kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 7 ya Mwaka 2015, ninaziagiza Kamati za Usimamizi wa maafa ziwajibike kutekeleza, kusimamia na kuchukua hatua zifuatazo;
"Kuhakikisha mvua hizi zinatumika kwa shughuli za maendeleo ikiwemo kilimo, kuandaa mabwawa na malambo kwa ajili ya kuvuna maji, kupanda mazao yanayohitaji maji mengi kama vile mpunga, uzalishaji wa samaki, kuandaa malisho na nyasi za akiba za mifugo.
"Pili kuandaa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu na wanyama kama homa ya matumbo na kipindupindu na magojwa ya milipiko ya mifugo.
"Tatu, idara na taasisi zinazohusika na mazingira na miundombinu, zihakikishe barabara zinapitika wakati wote na mitaro, makalvati na madaraja yanaimarishwa na kusafishwa ili kuruhusu maji kutiririka.
"Nne sekta za maji na umeme ziweke mipango kuhakikisha madhara katika huduma za maji na umeme yanapewa ufumbuzi mapema.
"Tano, kuainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa kwa kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake Ili kukabili maafa na kurejesha hali kwa wakati endapo maafa yatatokea,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt.Chana.
Hatua nyingine amesema ni kushirikisha wadau wa maafa kwa maana ya wananchi, taasisi na sekta binafsi katika mipango yote ya usimamizi wa maafa.
Pia amesema,wananchi wahimizwe kuishi katika makazi na kutekeleza shughuli za uzalishaji katika maeneo salama.
Mheshimiwa Waziri amesema kuwa, kumekuwa na matukio ya mvua zinazonyesha katika mikoa mingine kusababisha madhara katika mikoa ambayo hakujanyesha mvua.
Amesema, hali hiyo inatokana na hali halisi ya maumbile ya nchi yetu kuwa na mabonde ya mito mikubwa ambayo kwa sasa inapokea maji mengi kutoka milimani na pia uwezekano wa kujaa kwa mabwawa hali ambayo inaweza kupunguza kasi ya maji.
"Hivyo, wananchi wote wanaoishi na kuendesha shughuli za kiuchumi pembezoni mwa mabonde ya maji wanatahadharishwa kuchukua hatua ili kunusuru maisha na mali zao.
"Ikumbukwe kuwa madhara yanaweza kuongezeka endapo hatua stahiki hazitachukuliwa kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu. Vilevile, pamoja na madhara yanayoweza kujitokeza, umma unakumbushwa kutumia mvua hizi vizuri ili ziwe na manufaa kupitia shughuli za uzalishaji mali kama kilimo, kuandaa mabwawa na malambo kwa ajili ya kuvuna maji, kupanda mazao yanayohitaji maji mengi kama vile mpunga, uzalishaji wa Samaki, kuandaa malisho.
"Napenda kutoa wito kwa kila mwanachi, kaya pamoja na Kamati katika ngazi za mtaa au kijiji, wilaya na mkoa kuhakikisha kuwa tunatimiza wajibu wetu katika suala zima la kushughulikia maafa kwa mujibu wa sheria ili msimu huu wa mvua usiathiri maendeleo ya taifa letu.
"Aidha, Serikali itaendelea kuuarifu umma hatua za kuchukua kupitia taasisi husika na vyombo vya habari kwa kadri Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania itakavyokuwa ikitoa utabiri wake kwa vipindi mbalimbali,"amesema.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri amesema kuwa,utabiri uliotolewa unaonesha kuna uwezekano wa kuwa na ongezeko la mvua katika kipindi cha mwezi Machi katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na mwezi Aprili kwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.
Amesema,hali hiyo inaweza kusababisha madhara katika sekta mbalimbali ikiwemo mtukio ya magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama na wadudu waharibifu wa mazao na mimea yanaweza kujitokeza kutokana na hali ya unyevunyevu, kutuama kwa maji na kuchafuka kwa maji.
"Ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi na kuathiri shughuli mbalimbali hususani katika maeneo ya wachimbaji madini wadogo.
"Vipindi vya mvua kubwa vinaweza kuambatana na mafuriko na kusababisha uharibifu wa miundombinu, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali.
"Hivyo, wananchi wote mnaombwa kufuatilia kwa makini tahadhari na kutumia taarifa za wataalam kutoka sekta mbalimbali kwa usahihi na kuchukua hatua stahiki kwa ustawi wa uchumi wa nchi yetu.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri ametoa pole kwa wale wote ambao walipitia kipindi kigumu kutokana upungufu wa mvua za Vuli (Oktoba, Novemba na Disemba 2021) kwa mikoa inayopata misimu miwili kutokana na uhaba wa malisho na maji kwa mifugo.
Amesema, hali hiyo imesababisha baadhi mifugo kudhoofika na kufa kutokana na njaa na magonjwa nyemelezi. "Serikali inatoa pole sana kwa wale wote mliopata madhara.Aidha, niwapongeze kwa hatua mlizochukua kukabiliana na hali hiyo.
"Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu shughuli za maafa kwa kuhakikisha ushiriki wa Wizara, Idara, Taasisi, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa, asasi zote zisizo za kiserikali pamoja na umma kwa jumla katika kuzuia, kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 7 ya Mwaka 2015,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Balozi Dkt.Chana.