NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Benki ya CRDB itawapatia wajasiriamali mikopo bila riba na itahakikisha kiwango kinachokopwa ndicho kinachopaswa kurejeshwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika Uzinduzi wa Ushirikiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Benki ya CRDB kupitia Mikopo ya Wajasiriamali ya Inuka na Uchumi wa Buluu,hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mikopo kwa wajasiriamali ikiwa ni ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya CRDB, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar.
Katika hotuba yake Rais, Dkt. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo inatokana na ahadi yake na kusisitiza kwamba jambo la msingi ni kuzingatia vigezo na masharti yaliyopo ili kuhakikisha kwamba, wale wananchi wanaokopeshwa fedha hizo ni wajasiriamali halisi.
Aliongeza kuwa vile vile wana uwezo na taaluma ya ujasiriamali, waadilifu na wana dhamira ya dhati ya kurejesha fedha hizo.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa imani yake ni kwamba wajasiriamali wote watatoa ushirikiano mzuri kwa Benki ya CRDB na watachangamkia ipasavyo fursa zilizopo kwa kuzingatia taratibu zinazoongoza na kusimamia mikopo hiyo.
Alitoa pongezi na shukurani kwa uongozi wa Benki ya CRDB kwa kukubali kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwawezesha wajasiriamali na kuendeleza uchumi kama ilivyodhamiria.
Pia, alitoa pongezi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kushirikiana vizuri na taasisi husika katika usajili na uhakiki wa vikundi mbali mbali vya wajasiriamali na kuwataka kuendelea na zoezi hilo kwa misingi ya uadilifu.
Rais Dkt. Mwinyi alisisitiza kwamba Serikali haitomvumilia Kiongozi yoyote ambae atachangia au atashiriki katika wizi au upotevu wa fedha.
Hivyo, aliwataka viongozi hao kuhakikisha kwamba wale wanaowasajili kweli wametimiza vigezo, waadilifu na watatimiza masharti yaliyopo na kutoa wito kwa vikundi ambavyo havikupata fursa hiyo kwa kukosa sifa zilizotakiwa katika uhakiki wa awali wafanye maboresho ili nao wapate sifa ya kustahiki kupata mikiopo hiyo kama wenzao.
Alitoa shukurani za dhati kwa uongozi wa Benki ya CRDB kwa kuanzisha programu maalumu inayoitwa “INUKA” kwa lengo la kuhamasisha wajasiriamali kuchangamkia fursa za kiuchumi kupitia “UCHUMI WA BULUU”.
Alisema kuwa juhudi zinazofanywa na Benki ya CRDB katika kujenga uchumi wa Zanzibar ni nyingi na anaamini kwamba sasa zinafahamika vizuri na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika na kudumisha uhusiano mwema uliopo kwa faida ya pande zote mbili pamoja na wateja wote kwa jumla.
Alieleza kwamba mikakati ya Serikali ya kuwawezesha Wajasiriamali aliyoahidi sasa inatimia ikiwa ni pamoja na utoaji wa vitambulisho, ujenzi wa masoko, utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu, elimu, zana, mitaji, maeneo bora ya kufanyia kazi pamoja na utaratibu mzuri wa ulipaji kodi.
Aliwaahidi wajasiriamali kwamba Serikali itaendelea na juhudi za kuwapatia mitaji, masoko, elimu pamoja na kuweka mazingira rafiki ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Aliwasisitiza wale wate wanaojishughulisha na shughuli zao za ujasiriamali katika masoko ambayo yanakusudiwa kujengwa ni vyema wakapisha ujenzi huo na kuwaahidi kwamba wao ndio watakuwa wa mwanzo baada ya kukamilika ujenzi wa masoko hayo kukabidhiwa sehemu zao za biashara.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Serikali imeridhia na imekubali kutiliana saini na kuikabidhi kazi ya kusimamia utoaji na uendeshaji wa mikopo hiyo ambapo katika hatua ya awali Serikali imeamua kuweka katika benki ya CRDB zaidi ya TZS Bilioni 60 kati ya bilioni 81.4 kwa ajili ya kuanza mikopo.
Alisisitiza kwamba kati ya fedha za sekta ya uchumi wa Buluu, jumla ya TZS bilioni 20.34 zimeelekezwa kwa ajili ya ununuzi wa boti ambapo jumla ya boti 577 zinatarajiwa kununuliwa.
Vile vile, Rais Dk. Miwnyi alisema kuwa makundi mengine yatakayonufaika na fedha hizo ni wafanyabiashara wadogo wadogo, watengenezaji wa bidhaa mbali mbali, waendesha bodaboda, wahunzi, mafunzi seremala, Mama na Baba lishe, pamoja na wachora hina huku akiwataka Wakuu wa Wilaya kuhakikiihsa kundi la wachora hina lalikosi mkopo huo.
Nae Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban ambaye pia, ni Kaimu Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwezeshaji alisema kuwa malengo ya mikopo hiyo ni kuwapatia mitaji wajasiriamali wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi ili kuongeza mzunguko wa fedha ambao umeathirika na maradhi ya UVIKO 19, kuongeza fursa za ajira kwa jamii pamoja na kuongeza kipato cha wananchi na taifa kwa ujumla.
Alieleza kwamba zoezi la kuvitambua na kuangalia hali halisi ya vikundi lilifanyika kwa kushirikiana na sekta mbali mbali ambapo jumla ya vikundi 3494 ambavyo Unguja ni1915 na Pemba 1779 vimetambuliwa na kuangaliwa hali halisi ya vikundi hivyo.
Waziri Shaaban alisema kuwa kati ya hivyo vikundi 2,907 Unguja 1474 na Pemba 1433 vimeweza kuendelea na mchango wa upatikanaji wa mikopo ambapo vikundi 587 Unguja 105 na 482 Pemba vinahitaji kuimarishwa zaidi ili viweze kukidhi vigezo na kuweza kukopesheka na zoezi la kuviimarisha linaendelea.
Alisema kuwa baada ya kuthibitishwa orodha ya vikundi vitakavyopatiwa mikopo, vikundi hivyo vimeanza kupatiwa mafunzo ya awali kabla ya kupatiwa mikopo kwa lengo la kuwatayarisha juu ya utumiaji na urejeshaji wa mikopo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Mussa Msekela kwa upande wake alieleza kwamba katika kuhakikisha inasaidia maono ya Rais Dk. Mwinyi Benki ya CRDB imekuja na programu inayoitwa “INUKA”.
Aliongeza jinsi benki hiyo ilivyoanza mashirikiano yake na Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi kwa kuwasaidia wajasiriamali pamoja na miradi mbali mbali ya maendeleo Unguja na Pemba.
Mapema, Rais Dk. Mwinyi alitembelea mabanda ya Wajasiriamali na kupata maelezo kutoka kwa wajasiriamali hao jinsi wanavyofanya shughuli zao pamoja na kueleza mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo katika shughuli zao hizo.