NA GODFREY NNKO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amemteua Kanali Burhani Zuberi Nassoro kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 22, 2022 na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Mhandisi Zena A.Said.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi wa Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo umeanza leo Februari 22, 2022.
Kuhusu mamlaka
Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Namba 8 ya mwaka 2021 imeipa mamlaka uwezo kamili wa kupeleleza, kukamata, kuchunguza na hatimae kupeleka Mahakamani mashauri yanayohusiana na dawa za kulevya pamoja na makosa mengine yanayofanana nayo.
Aidha, sheria hii imefuta taasisi iliyokuwa ikisimamia uratibu wa masuala ya dawa za kulevya nchini ambayo ni Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kuanzisha taasisi inayojulikana kama Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, itakayoongozwa na Kamishna Mkuu na itakuwa chini ya Baraza la Taifa la Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ambalo linaongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Tofauti ya Sheria hii na ya zamani
Kwa ujumla sheria hii mpya kwanza, imeanzisha mamlaka yenye nguvu ya kisheria na thabiti ya kusimamia udhibiti wa dawa za kulevya nchini ambapo taasisi hii mpya ina uwezo wa kuchunguza, kukamata, kupeleleza na kufungua mashtaka mahakamani;
Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa anaweza kuhoji, kupeleleza au kufanya ukaguzi kwa mtu yeyote au kikundi chochote cha watu kadri atakavyoona inafaa;
Pia Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa, atakuwa na uwezo wa kukagua, kupekuwa, kuzuia, kukamata, kuweka kizuizini na kufanya uchunguzi kuhusiana na makosa yaliyo chini ya sheria hii;
Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa ambaye ana sababu za msingi za kuamini kwamba gari, ndege, meli, chombo cha kubebea mizigo au chombo kingine chochote cha usafiri kimetumika au kinatumika katika kutenda kosa chini ya sheria hii, anaweza kukisimamisha, kuingia na kuifanyia upekuzi gari, ndege, meli, chombo cha kubebea mizigo au chombo kingine cha usafiri na anaweza kwa madhumuni hayo kuvunja au kufungua mlango na kuondoa kizuizi cha kuingia ndani ya chombo;
Endapo mtu anachunguzwa au anashitakiwa kwa kosa chini ya Sheria hii, Kamishna Mkuu anaweza, pale ambapo anaamini kwamba ushahidi wowote unaohusiana na kosa au mali unapatikana katika akaunti ya benki, kufanya maombi mahakamani ya amri ya kuzuia akaunti ya benki;
Bila ya kujali masharti ya sheria yoyote, Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa anaweza wakati wowote kwa madhumuni ya Sheria hii kufanya uvamizi na kuingia katika jengo lolote ambalo anaamini kwamba kosa limetendeka au litatendeka ndani ya jengo hilo;
Sheria imeanzisha Baraza la Taifa la Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ambalo linaongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Baraza linasimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na ndio chombo kikuu cha maamuzi na lenye usimamizi wa jumla kwa mamlaka hii.
Kwa sheria hii, mamlaka inaweza kutoa maelekezo pale itakapohitajika kwa taasisi yoyote ya Serikali au idara katika kutekeleza masharti ya Sheria hii, na taasisi au idara hiyo itawajibika kutekeleza maelekezo hayo;
Sheria hii pia imetoa majukumu ya jumla kwa taasisi za umma katika kuzuia na kupambana na dawa za kulevya nchini, Baraza litapokea na kuzipitia taarifa za taasisi za umma juu ya majukumu yao katika kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Taasisi hizo ni:
(a) Idara ya Usalama wa Taifa Zanzibar;
(b) Jeshi la Polisi Zanzibar;
(c) Chuo cha Mafunzo Zanzibar;
(d) Ofisi ya Uhamiaji Zanzibar;
(e) Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar;
(f) Shirika la Bandari Zanzibar;
(g) Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali;
(h) Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu; na
(i) Taasisi nyingine yoyote kama Baraza litakavyoona inafaa.
Lengo la ujumla la sheria Namba 8 ya 2021 ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar;
Sheria hii imelenga kudhibiti makosa mbalimbali yanayohusu uhalifu wa dawa za kulevya na makosa yanayofanana nayo ambapo jumla ya vifugu 26 vimekataza moja kwa moja uhalifu wa dawa za kulevya pamoja na makosa yanayofanana nayo kama:
>Sheria inaharamisha mambo mbalimbali ikiwemo kilimo cha bangi, mirungi, kulima, kumiliki, kusafirisha, kuuza na kununua mbegu zinazoweza kuzalisha dawa za kulevya kwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha.
>Kufadhili biashara ya dawa za kulevya adhabu ya kifungo cha maisha na kutaifisha mali zote.
>Inaharamisha usafirishaji wa dawa za kulevya, kujihusisha kwa namna yoyote kinyume cha Sheria na kemikali zinazoweza kuzalisha dawa za kulevya kwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha.
>Inaharamisha kumiliki mashine, vifaa na maabara kwa lengo la kutengeneza dawa za kulevya kwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha na kutaifisha kifaa hicho Pamoja na mali.
>Mmliki wa jengo kuruhusu jengo litumike kwa uhalifu wa dawa za kulevya, adhabu ni Faini isiyopungua milioni 10 au kifungo kisichopungua miaka 30 au adhabu zote mbili.
>Sheria imekataza bila ya kuwa na kibali kuingiza, kutoa, kusambaza, kumiliki na kutengeneza kemikali bashirifu, adhabu ni kifungo kisichopungua miaka 30.
>Sheria imetoa adhabu kwa mtu yoyote atakekataa kutoa taarifa ama ushahidi unaohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya au kutoa taarifa za uongo kulipa faini isiyopungua shilingi milioni 30 na isiyozidi shilingi milioni 50 au kifungo kisichopungua miaka 15 na kisichozidi miaka 30 au adhabu zote mbili.
>Sheria imekataza kwa namna yoyote ile kusaidia au kusababisha kutendeka au kutenda uhalifu wa dawa za kulevya na kutoa adhabu sawa sawa na mtenda kosa mwenyewe.
>Sheria imekataza kutoa dawa tiba zinazotumika kwa matibabu ambazo zinaweza kutumika kama dawa za kulevya zinazozibitiwa kisheria kinyume cha utaratibu, inadhibiti matumizi ya dawa adhabu ni faini isiyopungua Shilingi Milioni Hamsini za Kitanzania au kifungo kisichopungua miaka thelathini au vyote viwili.
>Sheria imekataza kutumia dawa za kulevya, na akitiwa hatiani, atalipa faini isiyopungua Shilingi Milioni Tano za Kitanzania au kifungo cha mwaka mmoja au vyote viwili.
>Endapo mtu atajitayarisha au atajaribu kufanya au kutokuzuia kitu kinachosababisha utendaji wa kosa chini ya Sheria hii, atapewa nusu ya adhabu ambayo angestahiki kupewa endapo angetenda kosa hilo.
>Mtu atakayekiuka masharti ya kifungu chochote cha Sheria hii, kanuni yoyote au amri yoyote iliyowekwa chini ya Sheria hii ambapo adhabu yake haikutajwa, ametenda kosa, na akitiwa hatiani atatumikia kifungo kisichopungua miaka kumi na tano na kisichozidi miaka thelathini.
>Endapo daktari wa binaadamu, daktari wa meno au daktari wa upasuaji wa wanyama, ametiwa hatiani chini ya Sheria hii, bila ya kujali masharti ya sheria nyengine yoyote, jina lake litafutwa katika daftari la usajili na hatofanya kazi ndani ya Zanzibar.
>Endapo kosa limefanywa na kampuni chini ya Sheria hii, mtu ambaye, wakati kosa linafanyika, alikuwa dhamana na ana jukumu la kusimamia uendeshaji wa shughuli za kampuni, atachukuliwa kuwa ametenda kosa na, akitiwa hatiani atawajibika.
>Pale ambapo kosa lolote limefanywa na kampuni na imethibitishwa kwamba kosa limefanywa kwa kuridhiana au kukubaliana au limechangiwa na uzembe wowote kwa upande wa mkurugenzi, meneja, katibu au ofisa mwengine wa kampuni, mkurugenzi, meneja, katibu au ofisa mwengine huyo wa kampuni atashtakiwa na kuadhibiwa ipasavyo na kampuni hiyo itafutiwa usajili au kutaifishwa.
>Mmiliki, mkaazi au mtu anayehusika na usimamizi wa eneo atatakiwa kutoa taarifa haraka iwezekanavyo kwa Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa juu ya uwepo, ndani ya eneo lake, wa mimea ya dawa za kulevya, mazao ya dawa za kulevya au dawa za kulevya ambazo huenda zimelimwa, zimezalishwa au zimetengenezwa isivyohalali.Ikiwa mmiliki, mkazi, au mtu anayehusika na usimamizi, ameshindwa kutoa taarifa, ametenda kosa, na akitiwa hatiani, atalipa faini isiyopungua Shilingi Milioni Kumi za Kitanzania na isiyozidi Shilingi Milioni Hamsini za Kitanzania au kifungo kisichopungua miaka kumi na tano na kisichozidi miaka thelathini au vyote viwili.
>Mtu ambaye kwa makusudi au kwa nia ovu anatoa taarifa za uongo zinazosababisha ukamataji au upekuzi chini ya Sheria hii, ametenda kosa, na akitiwa hatiani, atalipa faini isiyopungua Shilingi Milioni Kumi za Kitanzania au kifungo kisichopungua miaka miwili au vyote viwili.
>Ufilisi wa Mali; Endapo mtu yoyote ametiwa hatiani kwa kosa chini ya Sheria hii, au atatiwa hatiani kwa kosa linalofanana nalo, na Mahakama ya jinai nje ya Zanzibar, mali anazomiliki yeye mwenyewe au mshirika wake, alizozipata kutokana na dawa za kulevya katika tarehe ya mashtaka au baada ya tarehe hiyo zitafilisiwa na kuwa mali za Serikali.
>Endapo mtu atatiwa hatiani na Mahakama nje ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria yoyote inayofanana na masharti ya Sheria hii, atashughulikiwa kama vile ametiwa hatiani na Mahakama yenye uwezo Zanzibar.
>Kitu chochote kilichotumika kwa ajili ya kufichia dawa za kulevya ambazo zinatakiwa kutaifishwa chini ya Sheria hii, kitu hicho kitataifishwa.
>Endapo mtu ameuza dawa za kulevya ambazo anafahamu au ana sababu ya kuamini kwamba dawa za kulevya zinatakiwa kutaifishwa chini ya Sheria hii, mapato ya mauzo yatataifishwa.
>Endapo mtu atamiliki kitu au mali iliyopatikana isivyo halali ikiwa yeye mwenyewe au mtu mwengine yoyote kwa niaba yake kinyume na sheria hii, kitu au mali hiyo itafilisiwa na Serikali.
>Kamishna Mkuu au ofisa aliyeidhinishwa anaweza kutoa amri ya kuzuia kitu au mali wakati wa kufanya uchunguzi, upelelezi au ufuatiliaji chini ya sheria hii, ikiwa anayo sababu ya kuamini kwamba kitu au mali yoyote kuhusiana na uchunguzi, upelelezi au ufuatiliaji uliofanyika imepatikana isivyo halali na kitu au mali hiyo kinaweza kufichwa, kuhaulishwa au kutumiwa kwa namna ambayo inaweza kuharibu utaratibu wa utaifishaji wa kitu au mali hiyo chini ya Sehemu hii.