NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Mzee John Malecela kufuatia kifo cha mpendwa wao Dkt.Mwele Ntuli Malecela.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari Ikulu ya Zanzibar, pia Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ametoa salamu hizo za pole kwa ndugu jamaa na marafiki pamoja na uongozi wote wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ambapo marehemu hadi umauti unamfika alikuwa ni Mkurugenzi wa Udhibiti wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele.
Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kusikitishwa na kifo hicho na kuwasihi ndugu, jamaa na marafiki pamoja na uongozi wote wa WHO kuwa na subira na ustahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo.
Rais Dkt. Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi, Amin.
Marehemu Dkt.Mwele Ntuli Malecela alizaliwa Machi 26, 1963 ambapo katika uhai wake aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Tafiti za kiafya Tanzania (NIMRI) ambapo pia, aliwahi kuwania nafasi ya mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015