NA MWANDISHI DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kuondoa hofu na kuamini kuwa maoni, malalamiko na changamoto wanazotuma kwake kupitia Mfumo wa ‘Sema na Rais Mwinyi’ (SNR) zinamfikia na kufanyiwa kazi kikamilifu.
Mheshimiwa Dkt.Mwinyi ametoa ufafanuzi huo wakati alipofanya mazungumzo ya moja kwa moja na kituo cha Redio ya Swahiba Fm, kufuatia hofu iliyojengeka miongoni mwa wananchi kuwa taarifa wanazotuma zinachujwa kabla ya kumfikia.
Ameeleza kuwa, utaratibu huo umeleta mafanikio makubwa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, na kusema asilimia 67 ya masuala yote yaliyowasilishwa kupitia mfumo huo tayari yamefanyiwa kazi.
Rais Dkt.Mwinyi amesema, utaratibu huo ni mzuri na unamsaidia sana kwani isingekuwa rahisi kwake kupokea simu zote hizo na baadae taarifa hizo kufikishwa katika taasisi zinazohusika kwa ajili ya kupata ufumbuzi, hivyo akasisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kutumia mfumo huo wa SNR.