Rais mstaafu Dkt.Kikwete afunguka katika Usiku wa Madini

NA GODFREY NNKO

RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete amesema kuwa, kauli mbiu ya mwaka huu katika Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Uwekezaji Katika Sekta ya Madini inadhirisha nia ya Serikali ya kuifanya Sekta ya Madini iweze kutoa mchango unaostahili kwa Taifa.
Kauli mbiu hiyo ya "Mazingira Wezeshi kwa Maendeleo ya Sekta ya Madini" ilikuwa inaongoza mkutano huo wa siku mbili ambao ulifanyika kati ya Februari 22 hadi 23, 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere kilichopo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla maalum ya Usiku wa Madini uliofanyika usiku wa kuamkia leo katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam amesema kuwa, kauli mbiu hiyo inaonesha dhamira ya kuiwezesha Sekta ya Madini itoe mchango stahiki kwa maendeleo ya Taifa letu tofauti na miaka ya nyuma.

"Pia inahakisi azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu mpendwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kusimamia mabadiliko ya kisera, mabadiliko ya kiutawala ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini barani Afrika.
"Ninafarijika kuona dhamira hiyo ipo pia katika shughuli nyinginezo za kiuchumi na kijamii hapa nchini, lakini ili azma hii itimie, nchi yetu haina budi kuwa na sera zinazotabirika. Hakuna mwekezaji anayewekeza mahali ambapo alipoingia mmepa mashariti haya, anapoendelea katikati mnamwambia mmegairi.
"Sasa huyu mwekezaji anapofanya plans (mipango) yake ya investment (uwekezaji) anaijenga kwenye misingi ya masharti mnayompa sasa.Hata anapokwenda kuchukua mkopo benki anachukua kwa misingi ya masharti anayopewa. Endelea kumsikiliza Mheshimiwa Dkt.Kikwete hapa nchini;
 

Waziri Biteko

Awali, Waziri wa Madini Dkt.Doto Biteko amesema kuwa, Usiku wa Madini waliamua kuufanya kwa ajili ya kuwatambua wachimbaji madini wote nchini.

"Wachimbaji hawa kwa mwaka mzima, jambo wanalohubiriwa ni kuzingatia sheria, hili umekosea kuna faini, hili umekosea kuna hiki.Hawapati hata muda kidogo wa kuambiwa jambo jema, kwamba hongera umefanya vizuri,
"Tukaamua tutenge siku maalumu kwa ajili yao kwa ajili ya kuwatambua na kuwatia moyo, wale waliofanya vizuri, na iwe chachu kwa wengine waweze kufanya vizuri zaidi katika mwaka unaokuja,"amesema Dkt.Biteko.

Amesema kuwa, mafanikio yanayohubiriwa katika sekta ya madini yanatokana na juhudi za watu mbalimbali kwa kuweka msingi wa kuisimamia sekta hiyo ili iwe na manufaa makubwa kwa Taifa, hivyo wataendelea kuwathamini na kuwaheshimu viongozi wote waliotangulia katika kuisimamia wizara hiyo.

Pia amesema kuwa, mafanikio ya Sekta ya Madini yanatokana na maelekezo ya mara kwa mara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
"Mafanikio ya Sekta ya Madini, mtu anayestahili pongezi kubwa kuliko mtu yoyote ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Yeye amekuwa akitupa maelekezo ya mara kwa mara juu ya namna gani ya kuwasadia wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa. Ametuambia tuondoe kero kwenye sekta ya madini, lakini tuifanye sekta hii ifungamanishwe na chumi nyingine, ili uwepo wa madini ufanye sekta nyingine zichangamke.

"Kama kuna mahali fulani yanachimbwa madini, basi mkulima wa maeneo yale apate masoko ya kuuza bidhaa zake, ule utaratibu wa kuchukua bidhaa zote kutoka nje ya nchi na kuzileta wakati Watanzania wana uwezo wa kuzizalisha, Mheshimiwa Rais anakemea tabia hiyo kwa nguvu zake zote, anataka Watanzania wanufaike na uwepo wa madini hayo.Mheshimiwa Rais metuelekeza vile vile kwenye ajira zozote zinazozalishwa katika nchi hii,sekta ya madini nayo ichangie,
"Nataka niwahakikishie kwamba, wakati wote tutaendelea kwa nguvu zetu zote kusimamia maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Pili wanaostahili pongezi hizi ni watafiti wa sekta ya madini, wachimbaji wa madini, waongeza thamani wa madini, na wafanyabisahara wa madini, hawa ndiyo wamekubali na kuielewa sauti ya Mheshimiwa Rais, wamezingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Tunawapongeza sana kwa kushiriki katika uchumi huu, tutawaunga mkono na kuwasaidia,"amesema.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news