NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo Februari 20, 2022 amerejea nchini akiwa na habari njema kwa Watanzania.
Ni baada ya kufanya ziara ya siku kadhaa barani Ulaya katika nchi ya Ufaransa na Ubelgiji ambapo mambo mazuri kwa ajili ya kustawisha uchumi na kuharakisha maendeleo nchini yamefikiwa.
Ziara ya Mheshimiwa Rais Samia, imeangazia fursa mbalimbali ikiwemo huduma za kijamii, masoko na misaada ya kifedha kwa ajili ya kufanikisha mipango ya Serikali kukamilisha miradi ya maendeleo.
Akizungumza baada ya kuwasili leo Februari 20,2022 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo Ilala jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais Samia amesema, amefanikiwa kupata msaada wa fedha za Kitanzania zaidi ya shilingi trilioni moja ambazo zitatumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa miaka mitatu nchini.
Mheshimiwa Rais Samia amesema, fedha hizo ni sehemu ya Euro bilioni 55 zilizotengwa kwa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zimetolewa kwa ajili ya kukabiliana na athari ya UVIKO-19.
Amesema,mkutano wao wa Jumuiya ya Ulaya na Jumuiya ya Afrika ulikwenda vizuri, "Kwani, tulikuwa na kauli mbiu kwamba jumuiya mbili, lakini dira moja,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam waliofika kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Februari 20, 2022 mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi katika nchi ya Ufaransa na Ubelgiji. (Picha na Ikulu).
Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa,katika kauli mbiu hiyo kuna Euro bilioni 150 ambazo ni kinyang’anyiro kwa Afrika.
"Hii inamaanisha kuwa, atakayewahi kupeleka miradi ya maana ndiye atakayepata fungu kubwa. Nasi tunajitayarisha na tumeshapeleka michache tukiwa huko,”amesema Mheshimiwa Rais.
Pia amesema, amefanikiwa kusaini mkataba na kampuni itakayokuja kutekeleza mradi wa maboresho ya Teminal II katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliyojengwa na Ufaransa miaka mingi iliyopita.
“Walivyosema itashinda hata ile ya Terminal, karibuni watakuja na wataanza.Tulikuwa na mradi wa kujenga viwanja vya ndege Kigoma, Shinyanga na Pemba, pia kulikuwa na mradi wa Green Cities kwa mikoa ya Kigoma, Pemba na mji mwingine, fedha zao zilikwama, lakini tulishakwamua, mradi mmoja umeshatiliwa na mwingine utatiliwa (kusainiwa) hivi punde,”amefafanua Mheshimiwa Rais Samia Suluhu.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Samia amefanikiwa kupata fedha kwa ajili ya kumalizia njia za miradi ya mwendokasi pamoja na shughuli za kilimo nchini.
“Lakini kwenye mwendokasi tulizungumza wakauliza kwani haiwezekani Dar es Salaam au Dodoma kukawa na mabasi ya umeme? Nikawaambia inawezekana sana, kwa hiyo hilo lipo kwenye mazungumzo, nadhani miaka minne, mitano, sita ijayo tunaweza kuwa kama Ulaya,”amebainisha Mheshimiwa Rais Samia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam waliofika kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam leo tarehe 20 Februari, 2022 mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi katika nchi ya Ufaransa na Ubelgiji.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia amezungumzia mkataba wa fursa za masomo nchini Ubelgiji ambao utaweka msingi wa kunufaika zaidi ya vijana 20 kama ilivyo sasa nchini.
“Pengine idadi ya hizo nafasi itazidi na tumekubaliana hivyo, tunaendelea na mazungumzo mkataba tutasaini baadaye. Pia tulifanya mazungumzo na Ufaransa na wafanyabiashara wa Ubelgiji tukatiliana saini mikataba kadhaa ya ushirikiano na hivi karibuni tunategemea kupokea ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchi hizo ili waje kuona wapi wanaweza kuwekeza, pale ambapo sekta binafsi inaweza kuwekeza, Serikali hatuna haja ya kuweka pesa yetu,”amesema.
Aidha, Mheshimiwa Rais Samia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa mapokezi mazuri, "Nashukuru kwa mapokezi mazuri kweli mnanitia moyo, tulikuwa kwenye ziara Nchi mbili za Ulaya (Ufaransa na Ubelgiji), tulianza Ufaransa kwa mwaliko wa Rais Macron nadhani mliona nimekutana na Rais wa Ufaransa Macron, pia nimekutana na Wafanyabiashara wa Ufaransa,"amesema Mheshimiwa Raisa Samia.
Tags
Habari